November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtendaji afukuzwa kazi kwa rushwa

Na Esther Macha, TimesmajiraOnline, Mbeya

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,limeridhia kumfukuza kazi Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iwindi,Lubaha Sonje,baada ya kupatikana na hatua ya kupokea rushwa wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika Novemba 8,2024,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Ezekia Shitindi,amesema kuwa baraza hilo kwa pamoja limeridhia kumfukuza kazi mtumishi huyo, kwa kuwa tayari shauri lake lipo kwenye masuala ya nidhamu.

“Kwa namna yeyote mtumishi akipatikana na rushwa,adhabu yake ni kufukuzwa kazi.Kuanzia leo baraza,limeridhia kwamba mtumishi huyo si Mtendaji wa Halmashauri,kulingana na makosa aliofanya na alipopelekwa Mahakamani alikiri kosa na kulipa faini sh.500,000.amesema Shitindi na kuongeza:

“Ukilipa faini tayari unakiri kosa ulilofanya,na sisi tusingeweza kupingana na maamuzi ya Mahakama,kazi yetu ilikuwa kuthibitisha.Rai yangu kwa watumishi wengine,wajifunze kupitia kwa mtumishi huyu,“.

Hata hivyo Shitindi amesema Mtendaji huyo alikamatwa na TAKUKURU na kupatikana na rushwa,hivyo kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria na taratibu za kiutunmishi .

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Iwindi ,Mfisile Swila,amesema kuwa mtumishi huyo alikamatwa na TAKUKURU akiwa ofisini kwake na kesi hiyo kupelekwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela(3) au kulipa faini sh.500,00.

“Inaonekana wananchi katika mazingira yake waluenda TAKUKURU,ambapo Mtendaji huyo,alipokea rushwa akiwa ofisini,na ilikuwa siku ya Jumapili na kesi ikawa inaendelea mahakamani.Kesi hii ni ya mwaka 2021 sio ya leo,na hukumu imekuja kutoka mwaka huu, sasa kiutumishi ukishahukumiwa kifungo au faini na hujakata rufaa maana yake una kosa,”amesema Diwani huyo.

Mmoja wa wananchi Kata ya Iwindi Sabina Atuganile,amesema kuwa uamuzi huo ni mzuri utaleta fundisho kwa watumishi wengine,katika suala zima la utendaji kazi kwani baadhi yao wamekuwa wakitesa wananchi pale wanapohitaji huduma mbalimbali.