November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aomba taa za kuongozea magari kuwanusuru wanafunzi

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

Diwani wa Kata ya Kiseke Halmashauri  ya Manispaa ya Ilemela Mwevi Ramadhan,ameelekeza kilio chake kwa TARURA Wilaya ya Ilemela,kwa kuomba kuwekwe taa za kuongezea magari,barabara ya Sabasaba-Kiseke-Buswelu eneo la shule za msingi Juhudi na Kiseke,ili kuwanusuru wanafunzi takribani 3400 na ajali.

“Eneo hilo lina alama ya pundamilia lakini imeisha futika, nimejenga hoja sasa tuachane na alama ya pundamilia tupatiwe taa za kuongozea magari barabarani katika eneo hilo, suala hilo lichukuliwe kama dharura ili tuwaokoe wanafunzi hao,”alisema Mwevi.

Diwani huyo,ametoa kilio hicho Novemba 6,2024,katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025,amedai  kiasi kinachohitajika kuweka taa hizo haizidi milioni 25.

“Kilio changu kimekuwa cha muda mrefu, lakini TARURA kila wakati wamekuwa wakitoa  majibu kuwa kufikia mwakani watato fedha kwa ajili ya uwekaji wa taa hizo,kimsingi mwezi huo wa Julai sitakuwepo kama Diwani ukomo wetu ni Juni 2025,”.

Hivyo ameomba jambo hilo lifike hatua za mbele zaidi na lifanyike mara moja ili kuokoa watoto zaidi ya 3400,ambapo amedai kuwa wapo watoto waliomaliza katika shule hizo wamekuwa walemavu kutokana na kugongwa na magari katika eneo hilo wengine wapo shuleni wakiwa na majereha.

“Kuna wakati uwa wanajitahidi wanaleta Askari wa usalama barabarani,lakini wanakaa kwa muda mfupi,wakati wa mvua wanakuwa hawapo,wanafunzi wakitoka darasani wanavamia  barabara,hivyo  kugongwa na bodaboda,” alisema Mwevi.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TARURA Ilemela,Mhandisi Gavidas Mlyuka,alisema,wakati wa ujenzi wa barabara hiyo ya Sabasaba-Kiseke-Buswelu,usalama wa eneo la shule ya msingi Kiseke na Juhudi,ulizingatiwa kwa kujenga uzio,amatuta mawili ya kupunguza mwendo wa magari  na uwekaji wa alama ya  pundamilia(zebra).

“Ili kuimarisha usalama zaidi katika  eneo hilo kuna uhitaji wa kuweka taa za kuongozea magari na watembea kwa miguu.Utekelezaji wa uwekaji wa taa hizo umepangwa kuwekwa katika kipaumbele cha bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2025/2026,”alisema Mhandisi Gavidas.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri  ya Manispaa ya Ilemela Ummy Wayayu,alisema,atashirikiana na TARURA,ili waone utekelezaji wa uwekaji taa hizo upoje.

“Tumelipokea  kama  taasisi,tutafanya mawasiliano na TARURA tuone  kama wana bajeti ya kutekeleza au la,au sisi kama Halmashauri tunalitekelezaje, kwani ni suala muhimu  kwa upande wangu nimelichukua,”.