Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Muasisi wa Jukwaa la Maonyesho na Tuzo za Mitindo za Swahili maarufu kama “Swahili Fashion Week & Awards” Mustafa Hassanali anatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa Mitindo wa BRICS+ unaofanyika Moscow kuanzia tarehe 3 – 5 Oktoba mwaka huu.
Mkutano huu wa kimataifa na wa aina yake kwenye masoko ya mitindo yanayochipukia utafanyika Moscow na unatarajiwa kuleta pamoja viongozi wa sekta, wakuu wa vyama vya mitindo, wazalishaji, wabunifu, na wataalam kutoka duniani kote kujadili mustakabali wa sekta ya mitindo.
Mkutano huo hutoa fursa za Biashara, Maonyesho ya Kimataifa ya urithi (heritage), ambayo hutoa tafsiri za kisasa za kiutamaduni katika muundo wa mitindo kutoka kote ulimwenguni, na hafla za elimu.
Ushiriki wa Mustafa Hassanali kwenye Mkutano wa Mitindo wa BRICS + unatoa fursa ya kukuza ushirikiano wa wataalamu wengi katika tasnia ya mitindo, kuimarisha uhusiano wa kitamaduni na biashara, na kushughulikia masuala makubwa yakiwemo uvumbuzi na maendeleo endelevu.
Mkutano wa BRICS+ ukiwa kama kiungo muhimu katika masoko ya mitindo yanayochipukia, utaangazia changamoto na mafanikio ya watu wenye vipaji, wabunifu, na makampuni ndani ya sekta hiyo.
Utaalam wa Tanzania katika mitindo na utamaduni utakuwa na thamani kubwa katika kusaidia bidhaa kutoka kwa vipaji chipukizi vya wabunifu kwa kiwango cha kimataifa.
Majadiliano ya mkutano pia yatazingatia mada kama vile utashi bandia (artificial intelligence), uwekezaji, na uzalishaji.
“Ninayo furaha sana kushiriki kama mwanajopo katika mkutano huu wa kimataifa unaofanyika Moscow, Urusi ninapoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na kuonyesha kazi za mshindi wa tuzo ya tuzo ya ubunifu Mugonzibwa Mkurugenzi wa NYUZI CAD kutoka Tanzania.
Tanzania ni miongoni mwa Nchi 93 zilizoalikwa katika Mkutano huu na Ushiriki Wangu utakuza na kuimarisha diplomasia ya Utamaduni na Uchumi” Alieleza Hassanali
Maonyesho ya Kimataifa ya Urithi “Heritage” yatakuwa kivutio kikubwa katika Mkutano huo. Yataonyesha ushawishi mkubwa wa urithi wa kitaifa na kitamaduni wa nchi wanachama wa BRICS, pamoja na nchi za Asia, Afrika, na Amerika ya Kusini juu ya mitindo ya kisasa na kujadili mwenendo wa kimataifa wa uhifadhi wa tamaduni katika muktadha wa kisasa.
Kufuatia Mkutano wa Mitindo wa BRICS +, Jukwaa la Maonyesho ya Mitindo la Moscow (Moscow Fashion Week) litafanyika Oktoba 4 hadi 9, likijumuisha wabunifu wenye vipaji kutoka Brazil, China, India, Indonesia, Urusi, Afrika Kusini, Costa Rica na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Mshindi wa tuzo mbalimbali Mustafa Hassanali ni mbunifu wa mitindo ambaye kazi zake zimeonyeshwa katika miji 33 na nchi 23 ulimwenguni. Yeye ndiye mwanzilishi na mratibu wa moja ya majukwaa makubwa ya maonyesho ya mitindo barani Afrika lijulikanalo kama Swahili Fashion Week & Awards na kwa sasa ni mwenyekiti wa Chama cha Mitindo Tanzania (Fashion Association of Tanzania).
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi