Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
VITA ya dawa za kulevya nchini yameonesha mafanikio makubwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mafanikio makubwa yaliyopatikana katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2023 yamekuwa ni makubwa na yakujivunia, kwani yameandika rekodi ambayo haijawahi kufikiwa kwa miaka 11 iliyopita.
Mwaka 2023 umekuwa wa kipekee sana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini, kwani Mamlaka ya Dawa za Kulevya imefanikiwa kukamata kiasi kikubwa cha dawa hizo kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mapambano ya dawa za kulevya hapa nchini.
Taarifa ya aliyekuwa Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, aliyoiwasilisha Bungeni, jijini Dodoma hivi karibuni, ilieleza kwamba mafanikio hayo yametokana dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia.
Alisema Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilifanikisha ukamataji wa jumla ya kilogramu 1,965,340.52 zikihusisha watuhumiwa 10,522 (wanaume 9,701 na wanawake 821).
“Dawa za kulevya zilizokamatwa ni kama ifuatavyo; Heroin
Kilogramu 1,314.28, Cocaine kilogramu 3.04, Methamphetamine Kilogramu 2,410.82, Bangi Kilogramu 1,758,453.58, Mirungi
Kilogramu 202,737.51, Skanka Kilogramu 423.54 na Dawa Tiba
zenye Asili ya Kulevya gramu 1,956.9 na mililita 61,672.” Alisema.
Aidha, kiasi hiki cha dawa za kulevya kilogramu1,965,340.52
zilizokamatwa katika kipindi cha Januari – Desemba 2023, ni
karibu mara tatu ya kiasi cha dawa za kulevya zilizokamatwa nchini
kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ambacho ni kilogramu 660,465.4.
Aidha, alisema dawa ngeni zilizoanza kuingizwa nchini hivi karibuni kama vile methamphetamine, skanka na biskuti zilizochanganywa na bangi pia zilikamatwa katika kipindi hicho.
Alisema katika kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanaimarishwa nchini, Serikali imenunu Boti yenye mwendo kasi (Speed Boat) ambayo pamoja na shughuli zingine itakuwa ikifanya doria baharini ili kufuatilia vyombo vinavyohisiwa kuingiza dawa za kulevya nchini kama vile Heroini, Methamphetamine na nyingine. Boti hii ilizinduliwa Aprili 28, 2024 Jijini Dar es Salaam
Boti hiyo mpya ya kisasa ina uwezo mkubwa wa kuhimili utekelezaji wa majukumu ya doria. Boti hiyo ya doria imepewa jina la Patrol Boat Sailfish (PB Sailfish).”
Uwepo wa boti hiyo utaleta mageuzi makubwa kwenye ulinzi na usalama wa baharini kwani itawezesha kufanya doria na kaguzi kwenye maji ya Tanzania.
Aidha, itafanya utafutaji na uokozi pindi zikitokea ajali baharini na kuimarisha ulinzi kwenye pwani yetu kwa kuwa imewekewa mitambo maalum ya silaha pamoja na mtambo maalum wa kuzima moto… boti hii ni mwarobaini wa kuhakikisha pwani ya Tanzania iko salama.”
“Uwekezaji huu mkubwa juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya na ukamataji mkubwa uliofanyika mwaka 2023, unadhihirisha dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia,” alisema.
Aliongeza kwamba Serikali imeendelea kuboresha huduma za tiba kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo.
Anasema hadi kufika Mwezi Desemba 2023, Serikali ilikuwa na vituo 16 vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics).
Vituo hivyo viliwahudumia waraibu wa dawa za kulevya 15,912. Aidha, Katika kipindi hicho kulikuwa na nyumba 56 za upataji nafuu (sober houses) zikihudumia waraibu 3,488.
Alisema Serikali ilisimamia kikamilifu uanzishaji na Uendeshaji wa nyumba hizi. Pia, tiba ya uraibu wa dawa za kulevya hutolewa kwenye vitengo vya afya ya akili vilivyopo katika
Hospitali za Wilaya, Mikoa na rufaa nchini.
Hadi kufikia Desemba mwaka 2023, jumla ya waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipatiwa huduma katika hospitali hizo.
“Hii ni hatua muhimu katika kupunguza madhara yanayotokana na
matumizi ya dawa za kulevya kama vile, Uraibu, UKIMWI, Kifua
Kikuu, Homa ya ini, Magonjwa ya akili na magonjwa mengine
yasiyoambukiza,” alisema.
Alisema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Taifa cha Utengamao kwa ajili ya kuwahudumia waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu.
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama hatua za mwanzo za ujenzi wa kituo hiki kinachojengwa katika eneo la Itega Jijini Dodoma zimeshaanza.
Aliongeza kwamba ujenzi wa kituo hicho utasaidia kuwajengea uwezo waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ili waweze kujikimu kimaisha na hivyo kutokurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Waziri Mhagama, alisema katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini, Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na wadau wengine, iliendelea kutoa elimu juu ya madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya katika jamii ili jamii isijiingize kwenye matumizi ya dawa hizo.
Alisema elimu hiyo ilitolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, mitandao ya kijamii, semina, makongamano, mikutano, vilabu vya kupinga rushwa na dawa za kulevya shuleni na vyuoni na maonesho mbalimbali ya Kitaifa na kimataifa ambapo karibu watu milioni 22.7 walifikiwa.
Alifafanua kwamba katika kipindi cha mwaka 2023, Serikali ilianzisha kituo maalumu cha Habari na Mawasiliano katika ofisi za Mamlaka ambapo, mwananchi yeyote anaweza kupiga simu namba 119 bila malipo ili kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya.
“Ukipiga namba hii pia unaweza kupatiwa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya pamoja na ushauri mwingine.
Hatua hii imesaidia kuongeza tija katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwani taarifa tunazozipata kupitia kituo hiki zimesaidia kuwakamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Natoa wito kwa wananchi wote kutumia namba hii kutoa taarifa kwa Mamlaka juu ya watu wanaojihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kupatiwa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya,” alisema Mhagama na kuongeza;
“Taarifa yako itafanyiwa kazi kwa usiri na utakuwa umeokoa jamii
ya kitanzania dhidi ya dawa hizi hatari.”
Katika kupanua wigo wa udhibiti dawa za kulevya nchini, Serikali
imefungua ofisi mpya tano za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana
na Dawa za Kulevya katika ngazi ya kanda.
Alisema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ofisi zake ziko Mkoa wa Mbeya inahudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa Njombe na Iringa.
Kanda ya Kaskazini ambayo ofisi zake ziko Mkoa wa Arusha inahudumia mikoa ya Arusha, Manyara Kilimanjaro na Tanga. Kanda ya Pwani Yenye ofisi katika Mkoa wa Mtwara, inahudumia Mikoa ya Pwani,
Alisema Mtwara, Lindi, Ruvuma na Morogoro; Kanda ya ziwa ambayo ofisi zake ziko Mkoani Mwanza inahudumia Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Simiyu na Shinyanga, pamoja na Kanda ya kati yenye ofisi Mkoani Dodoma inahudumia Mikoa ya Dodoma, Kigoma Singida na Tabora.
“Hatua hii imesaidia kupanua wigo wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini na kuleta mafanikio.
Serikali ina mpango wa kuanzisha ofisi za Mamlaka katika ngazi
za Mikoa ili kuimarisha mapambano dhidi ya dawa hizo.
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama tatizo la dawa za kulevya ni suala mtambuka linaloathiri nyanja mbalimbali zikiwemo za afya, uchumi, siasa, mazingira, diplomasia, jamii, usalama wa nchi na dunia kwa ujumla.
“Hivyo mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushiriki wa wadau wote nchini.
Serikali imetunga Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024 ili kuhakikisha kuwa wadau wote nchini wanashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya,” alisema.
Alisema Sera hiyo itaimarisha udhibiti wa dawa za kulevya zinazozalishwa nchini kama vile bangi na mirungi.
Sera inatoa maelekezo ya kufanya utafiti wa mazao mabadala katika
maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha mazao hayo ili wananchi wa
maeneo husika wajihusishe na kilimo cha mazao halali badala ya
kilimo cha bangi na mirungi.
Aidha, Sera inaelekeza kuwajengea uwezo wadau mbalimbali katika udhibiti wa dawa za kulevya ili ushiriki wao ulete tija katika mapambano haya.
Pamoja na mafanikio hayo, Waziri Mhagama anasema bado tuna safari ndefu katika kupambana na janga hili, kwani ni wazi kuwa bado dawa za kulevya zinaingia nchini kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika nchi zinazozalisha dawa hizi, kubadilika kwa teknologia za uzalishaji na usafirishaji pamoja na utandawazi.
Idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya nchini ni vijana kwa wastani wa asilimia 78, hivyo kuathiri nguvu kazi ya Taifa ambayo ni mhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mhagama alitoa rai kwa jamii kuwa, suala la elimu ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya linapaswa kuanzia ngazi ya familia.
“Wazazi na walezi tuendelee kuwajengea misingi bora watoto wetu
ili wasijiingize kwenye vitendo viovu na makundi hatarishi
yanayoweza kuwaingiza kwenye matumizi na biashara ya dawa za
kulevya.”Alisema.
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia