Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline,Dar
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kudhibiti maandamano ya CHADEMA linawashikilia watu 14 wakiwemo viongozi wa juu wa Chama kwa kujihusisha na maandamano yaliyopigwa marufuku na jeshi hilo.
Kukamatwa kwa watu hao kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana. Alisema watu hao wamekamatwa kwa kukaidi amri halali ya polisi ya kuacha kushiriki maandamano.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless lema.
“Jeshi la polisi lilifuatilia kwa ukaribu matamko mbalimbali ya viongozi wa chama hicho kuhamasisha maandamano hayo, kufuatia matamko Polisi ya kupiga marufuku maandamano.
“Kwa hiyo leo hii tumewakamata watuhumiwa hawa ambao walikaidi kwasababu ambazo tulizieleza na mahojiano yanaendelea,” alisema Muliro.
Aidha Kamanda Murilo alitoa wito kwa wananchi Dar es Salaam wasiwe na hofu na waendelee na shughuli zao mbalimbali za kiuchumi, kijamii ulinzi unaendelea kuimarishwa kwa kiwango cha juu.
“Jukumu la Jeshi la Polisi kikatiba, kisheria ni kuona watu wanaendelea kufanya shughuli zao bila hofu na kuhakikisha mali zao halali zinaendelea kulidwa,”alisema
Pia Kamanda Murilo alisisitiza kuwa taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba watu hao wametekwa sio za kweli bali wamekamatwa na wanahojiwa kwa mujibu wa Sheria kuhusiana na katazo Jeshi la Polisi lililotoa kuhusiana na maandamo.
“Kazi kubwa ya Jeshi la polisi Tanzania ni kuzuia matukio sio kusubiri mpaka yatokee watuhumiwa wamekamatwa Dar es salaam”alisema
****Mbowe alivyokamatwa
Mbowe alikamatwa na Polisi eneo la Magomeni, wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alizingirwa na Polisi. Alifika eneo hilo akiwa na gari dogo, kisha kuanza kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu lengo la maandamano hayo.
Mbowe, alisema wameamua kuweka mkazo wa maandamano baada ya maombi ya mahitaji, ikiwemo kutaka kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, viongozi waandamizi wa ulinzi na usalama kama sehemu ya uwajibikaji. Amesema jambo lingine waliloliomba ni kurejeshwa kwa viongozi wa chama hicho, waliotekwa kwa nyakati tofauti wakiwa hai au hali ya umauti, akiwemo Deusdetith Soka, Dioniz Kipanya, Jacob Mlay na Mbwana Kombo.
Aidha, Mtoto wa Mbowe, Nicole Mbowe, alikamatwa na Polisi wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari.
Nicole alikamatwa na polisi muda mfupi baada ya baba yake, Freeman Mbowe kukamatwa eneo hilo hilo la Magomeni.
***Lissu
Kukamatwa kwa Lisssu kulithibitishwa na Wakili wa CHADEMA, Hekima Mwasipu. “Lissu amekamatwa nyumbani kwake Tegeta na amepelekwa Kituo cha Polisi Mbweni na mimi kama wakili niko njiani nakwenda huko kujua sababu za kukamatwa kwake,” alisema Hekima.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa