September 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Igunga kuwa kitalu cha uzalishaji mbegu za mpunga

Na Lubango Mleka, TimesMajira Online – Igunga

Shamba linalomilikiwa na Ushirika wa Umwagiliaji mpunga Mwamapuli,linatarajiwa kuongezewa eneo lenye ukubwa hekta 1,557,huku sehemu ya hekta hizo zitatengwa kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora za zao la mpunga.

Ambapo wakulima wa .punga katika Skimu ya Umwagiliaji Mwamapuli kijiji cha Mwanzugi Kata ya Igunga wanatarajia,kupata mbegu bora za zao la mpunga zitakazozalishwa katika shamba hilo.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe,akizungumza na wakulima wa mpunga na wataalamu wa kilimo,baada ya kufanya ziara ya kukagua skimu za umwagiliaji na mabonde ya mpunga yaliyopo wilayani hapa,amesema sehemu ya eneo hilo,wapewe wataalamu wa kilimo ASA, TARI na Tumbi, kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora.

“Tutaweka hapa kituo,na mtafundisha utaratibu mpya wa namna ya kupanda, ili kupunguza kilo za mbegu tunazotumia kwenye upandaji,kwani wakulima wengi wa mpunga, wanatumia gharama kubwa ya mbegu kwa sababu ya kutopata utaalamu,” amesema Bashe.

Bashe amesema,ujenzi huo mpya wa skimu utakwenda sambamba na ujenzi upya wa bwawa ambalo limekuwa ni la muda mrefu, nyumba ya ofisa kilimo katika eneo la skimu, ghala jipya la kisasa la kuhifadhia mpunga, ofisi mpya za ushirika na muundo mpya wa uendeshaji ushirika.

Pamoja na kituo cha zana za kilimo ambacho zitawekwa kubota (power tilla) na mashine za kuvunia (combine havest),zitakazofanya kazi kwa bei ya Serikali pamoja na mashine ya kisasa ya kukoboa mpunga.

Katika hatua nyingine,amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo na Mkurugenzi mytendaji wa hyalmashauri ya wyilaya ya Igunga, Selwa Hamid ,kuweka uzio katika eneo la skimu ili kuzuia mifugo kula mazao ya wakulima,kwani ni kilio cha muda mrefu.Pia kuzuia ujenzi holela wa nyumba katika mabonde ya kilimo.

Awali, Meneja wa Chama cha Ushirika na Umwagiliaji mpunga Mwamapuli, Nkwabi Igesse, amesema kuwa eneo linalomwagiliwa ndani ya skimu ni hekta 630 zilizosanifiwa kwa wakati huo kupata maji.mwaka 1985 Serikali kwa kushirikiana na wahisani kupitia mfuko wa maendeleo ya umoja wa mataifa (UNGCF) na benki ya maendeleo Afrika (ADB) walijenga mfereji wa kwanza (primary canal) wenye urefu wa mita 2, 865 na wapili (secondary canal) wenye mita 11, 03 ambayo haikusakafiwa na ujenzi wake ulikamilika mwaka 1994.

“Ushirika wetu una wanachama 970, kati ya hao 270 ni wanawake na wanaume 700, kupitia kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika wakulima wemeongeza uzalishaji kutoka tani 2.5 za mpunga hadi kufikia tani 7.5 kwa hekta moja, lakini pia skimu inavikundi vya nje ambavyo hupata maji kupitia utaratibu uliopangwa kwa wakulima zaidi ya 3 000,” amesema Igesse.

Pia amesema,ushirika huo unamiliki trekta moja, ‘combating havest’ moja na mashine ya kukoboa mpunga moja, huku changamoto ikiwa ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya mifereji, barabara za shambani, madaraja na milango ya kufungia maji,wafugaji kuingiza mifugo na kulisha mazao.Pamoja na kuharubu miundombinu ya skimu, ukosefu wa hati miliki ya shamba na majengo ya chama.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mdolwa amesema kuwa, mwaka 2023 mwishoni walipata maelekezo kutoka kwa Waziri Bashe kuwa skimu ya umwagiliaji mpunga Mwamapuli ipewe kipaumbele.Hivyo Tume hiyo ilifanya usanifu na kikamilisha,ambapo wametangaza kuanza kwa ujenzi ambapo ndani ya siku 14 zijazo watapata Mkandarasi ambaye ataanza ujenzi.

“Mkandarasi atajenga ofisi kwenye mradi huu, ujenzi wa nyumba ya msimamizi wa mradi, mifereji ya zenge mita 27,190, mapitio mita 34, 177, vigawa maji 40, maboksi ya karavati 7, paipu karavati 36,barabara za ndani ya shamba kilomita 38, ununuzi wa gari la msimamizi wa mradi, ujenzi wa hekta 1,557 ambazo hazikuwepo hivyo ukijumlisha na zile 630 zilizopo skimu itakuwa na jumla ya hekta 2,187,” amesema Mdolwa.

Mkulima Jumanne Rashid ,amesema,”Hili suala la Igunga kuwa kituo cha kilimo, nimelipokea kwa asilimia 100, kwa sababu tutakuwa na uhakika wa mbegu maana hizi za dukani nyingi hatuna uhakika nazo,” amesema Rashid.

Naye, Amani Nyamweko, amesema kuwa, kujengwa kwa bwawa la Mwamapuli,itasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao.Huku ujenzi wa mashine ya kisasa ya kukoboa mpunga itaongeza kipato kwa wakulima, maana watauza mchele wenye ubora na amemuomba Waziri Bashe kuwatafutia masoko ya nje pindi mashine hiyo itakapo kamilika.