October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ushauri wa bure kwa TFF kuhusu uzinduzi jina la Uwanja wa Mkapa

Na Philemon Muhanuzi, Times Majira Online

UWANJA wa Taifa kupewa jina jipya la uwanja wa Mkapa (Mkapa National Stadium) ni uamuzi sahihi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli.

Rais aliutamka hadharani uamuzi huo siku ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu hayati Benjamin William Mkapa pale katika jukwaa la uwanja wa uhuru.

Upo ujumbe maalum kwa TFF kama taasisi ambayo imekuwa ni mtumiaji mkubwa wa uwanja wa Mkapa.

Ni ushauri ambao ukisikilizwa na kufanyiwa kazi, TFF watakuwa wamejiongezea heshima sio kwa wapenda soka tu bali kwa Watanzania wote.

  1. Mechi ya kirafiki siku ya uzinduzi ni muhimu

Kauli ya Rais Magufuli ni agizo, lakini kiubinadamu na kwa heshima ni bora TFF wakaandaa mechi maalum kwa ajili ya kuzindua jina jipya la uwanja.

TFF kama watumiaji wa mara kwa mara wa uwanja huo, wanao wajibu wa kulitekeleza agizo la kiongozi mkuu kwa kufanya jambo lenye kuweza kutafsiriwa kama ni asante maalum kwa mwezeshaji wa ujenzi wa uwanja.

Mechi za Simba na Yanga zilizokwisha kuchezwa katika nyasi za uwanja wa Mkapa tangu mwaka 2008 zimeshaingiza mabilioni ya shilingi.

Mamlaka ya mapato TRA wamekuwa wakikusanya sehemu yao ya mgao wa kila mechi, pesa ambazo zimekuwa zikitumiwa katika uimarishaji wa shughuli mbalimbali za kijamii.

  1. Namba ya jezi mojawapo ya Taifa Stars istaafishwe

Upo umuhimu wa kumualika Mjane wa hayati Mkapa, Mama Anna Mkapa siku ya mechi hiyo ya kirafiki ya Taifa Stars. Kabla mechi haijaanza akabidhiwe jezi maalum yenye namba iliyostaafishwa kutumika.

Jezi hiyo iwe na jina la MKAPA nyuma yake na ikiwezekana pale pembeni ya bendera ya Taifa pawekwe namba tatu ikiwa ni utambulisho wa awamu aliyoiongoza Hayati Mkapa.

Mwaliko wa Mama Anna kwa heshima unaambatana na uwepo wa Rais mwenyewe au Makamu wake au Waziri Mkuu. Ni bora kwenye jambo hili familia ya Hayati Mkapa ikapewa taarifa za miezi kadhaa kabla ili ijipange.

Na pia ni bora mechi hii ya kuzindua jina ikachezwa baada ya uchaguzi wa mwaka huu kuwa umeshamalizika, kwa maana ya mapema mwakani au mwishoni mwa mwaka huu.

  1. Sanamu ya hayati Mkapa ijengwe ndani y uzio wa Uwanja

Huwa tunaviona viwanja vingi vikubwa duniani vikiwa na sanamu za watu maarufu zinazojengwa nje kidogo ya majukwaa lakini katika eneo la uwanja. Zinakuwa ni sanamu za viongozi wa nchi, wachezaji bora wa miaka ya nyuma au makocha walioacha rekodi nzito.

Naamini pale karibu na eneo la kuegeshea magari panaweza kujengwa sanamu ya Hayati Mkapa, kama kuheshimu ujasiri wa maamuzi yake ya kutenga mabilioni ya shilingi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wenye hadhi ya kimataifa.

Vijana wa miaka ya 2045-50 watakapokuwa wakiulizia hii sanamu ni ya nani, waweze kuambiwa kuwa ni ya kiongozi wa nchi aliyewezesha ujenzi wa uwanja huu.

Uwanja wa Mkapa umekuwa ukiwaduwaza wageni kutoka mataifa ya mbali wanaokuja kutazama mechi na hata wachezaji wamekuwa wakiusifia kwa uzuri ulionao.

Wachezaji wa timu ya Taifa ya Brazil wamezoea kucheza katika viwanja vikubwa vya kwao na vile vya Ulaya lakini walishangaa siku ile walipokuwa wanatoka vyumbani na kuelekea kujipanga katika mstari kabla mechi dhidi ya Taifa Stas haijaanza.

Wachezaji wa Ivory Coast iliyoongozwa na Didier Drogba walijikuta wakiushangaa uzuri wa uwanja siku ule walipocheza na Taifa Stars, mechi iliyochezwa kuanzia saa moja ya usiku.

TFF wajitathmini na wala wasikubali agizo la uwanja wa Taifa kubadilishwa jina na kuitwa uwanja wa Mkapa, likapita pasipo wao kurudisha shukrani kwa Hayati Mkapa, ambaye anaweza kuwakilishwa na Mjane wake Mama Anna.