November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ndumbaro ataka Watanzania kutunza, kuendeleza mila na desturi

Na Cresensia Kapingai, Timesmajiraonline Songea.

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Damas Ndumbaro, amewataka Watanzania kutunza na kuendeleza urithi wa tamaduni zetu, huku akiimiza wazazi kukemea mmomonyoko wa maadili kwenye nchini.

Agizo hilo alilitoa jana wakati akizinduaTamasha la Tatu la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika kwenye viwanja vya Maji Maji,Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.

Aliwataka Watanzania wasitumie haki za binadamu kukiuka miiko na kuharibu mila na desturi za nchi yetu.

“Lazima tufundishe mila na desturi za kitanzania na historia yetu kwa watoto kwani ni taifa la kesho,” alisema na kusisitiza;

“Watanzania tunapaswa kudumisha upendo, ushirikiano, utulivu na amani ambapo kupitia tamasha hili tutaweza kuelewa umuhimu wa amani na kufuata mila na desturi zetu ili kuondokana na utandawazi ambao hauna maana .

Tuwafundishe watoto wetu maadili mema, mila na desturi zetu na hata historia kwa kufuata kauli mbiu yetu ya “Utamaduni wetu ni utu wetu tuenzi na kuuendeleza. “

“Familia zimekuwa mstari wa mbele kulalamikia mmomonyoko wa maadili badala ya kutoa elimu kwa watoto wetu, taasisi za dini , watu maarufu na vyombo vya habari zikiwemo shule kuanzia ngazi ya chekechea hadi vyuo vikuu vitusaidie kupambana na mmomomyoko wa maadili.” alisema Dkt.Ndumbaro

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, alisema Mkoa wa Ruvuma unatambua umuhimu wa utamaduni na ndio maana hawakusita kuwa wenyeji wa Tamasha hilo la tatu la kitaifa la utamaduni .tunatambua umuhimu wa kukuza sanaa na michezo kwenye taifa hili.

Alisema, tamasha hilo ni fursa ya kukuza Uchumi wa Mkoa wa Ruvuma hivyo amewakaribisha wageni wote kutoka ndani na nje ya mkoa kutembelea vivutio vilivyopo kwenye mkoa wa Ruvuma .

“Nimefarijika kuona bado Mkoa wa Ruvuma tunaongoza kwa hivyo karibuni kwenye tamasha letu hili kubwa la kitaifa na mwendelee na shamra shamra kama kawaida kwani mkoa upo salama hivyo tunawakaribisha wananchi wote waje kushiriki,”alisema Rc Abbas.

Naye Naibu Waziri Wizara ya Utamaduni wa Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma alisema Tamasha hilo ni muhimu kwani litasaidia wananchi kukumbushwa mila na desturi za Mtanzania , hivyo itasaidia kuondoa ushoga na usagaji na litaendelezwa.

Alisema ,Tamasha la utamaduni la kitaifa linaendelea kukua mwaka hadi mwaka hivyo wataendelea kusimamia maelekezo ambayo yametolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwasaidia wananchi kufuata mila na desturi za Kitanzania.

Mwisho.