November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uboreshaji hospitali, kumepunguza rufaa kwa wagonjwa

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

SERIKALI imeeleza kuwa maboresho yaliofanyika katika hospitali za Rufaa za Mikoa nchini,yamesaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi, waliokuwa wanalazimika kusafiri nje ya nchi kufuata huduma za afya za kibingwa.

Kauli hiyo imetolewa Septemba 18,2024 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ,Juma Homera,wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Waganga Wafawidhi, Wauguzi Wafawidhi, Makatibu wa hospitali na Waratibu wa ubora wa huduma wa hospitali za Rufaa za Mikoa ya Tanzania Bara.Ambapo kikao hicho kimefanyika mkoani Mbeya.

Homera, amesema,uboreshaji wa vifaa, majengo na utaalamu katika hospitali za Rufaa za Mikoa,umewezesha wananchi kupata matibabu sahihi na kwa wakati.

Pia zimepunguza rufaa za wagonjwa, kwani huduma za kibingwa zipo kwenye mikoa, hivyo kuepuka gharama za ziada zilizokuwa zinasababishwa na ucheleweshaji wa huduma kutofanyika kwa wakati.

“Kwa sasa wananchi,wameweza kupata huduma za afya za kibingwa, ndani ya mikoa yao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali za Taifa au nje ya nchi, hii imepunguza gharama kwa wananchi,”amesema Homera na kuongeza:

Hata hivyo Mkuu huyo Mkoa, ametoa wito kwa Waganga Wafawidhi,kutumia vitengo vya habari,kutangaza kazi zilizofanywa na Serikali, ili wananchi wajue huduma zilivyoboreshwa na zinazotolewa katika hospitali hizo.

“Taasisi ina miradi mingi lakini cha kushangaza wananchi hawajui, hakikisheni mnakuwa na Maofisa Habari wanaojua majukumu yao.Hakuna sababu ya kuwa na watu wasiojua umuhimu wa kutangaza miradi inayotekelezwa na Serikali,”amesema Homera.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anaye simamia Huduma za Hospitali kutoka Wizara ya Afya Dkt. Caroline Damian, amesema lengo la serikali ni kuhakikisha uwekezaji uliofanywa una tafsiriwa katika huduma za afya,zenye ubora kwa wananchi wote wa Tanzania

“Miongoni mwa mikakati ambayo tunaenda kuweka kwa pamoja na kukubaliana baada ya kikao hiki,ni kuhakikisha tuna simamia utoaji wa motisha kwa watumishi wa sekta ya afya, ili waweze kufanya kazi kwa morali na kutoa huduma bora ikiwa ni pamoja na kuwalipa stahiki zao kwa wakati,”amesema Dkt. Carol.