Joyce Kasiki
MOJA ya jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita ni kuendelea kuboresha miundombinu ya jamii na hasa ikizingatia huduma ya makuzi bora ya mtoto .
Mnamo Disemba 2021 Serikali ilizindua Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya miaka mitano iliyolenga kutatua changamoto za watoto wenye umri wa 0 mpaka miaka minane kwa lengo la kuhakikisha kundi hilo la watoto linapata malezi stahiki kwa ajili ya kufukia hatua timilifu za ukuaji na kuleta tija katika Taifa.
Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt.Festo Dugange anasema katika eneo hilo serikali inaangalia makundi mawili likiwemo la mtoto kabla hajazaliwa yaani tangu kutungwa kwa ujauzito mpaka umri wa miaka mitano lakini pia inaangalia baada ya miaka mitano mpaka umri wa miaka 17.
Anasema katika hayo yote, umakini mkubwa upo tangu pale mama anaposhika ujauzito,kujifungua ,siku 1000 za kwanza mpaka miaka mitano ili kuhakikisha mtoto anakua vyema na kuleta tija katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Dkt.Dugange anasema,katika sekta ya afya serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu ya afya na hasa kwa kusogeza vituo vya huduma karibu na wananchi.
“Ikumbukwe changamoto kubwa sana ya huduma za afya katika nchi yetu ilikuwa ni watu kupata vituo vya kutolea huduma karibu na makazi yao ambapo wananchi walikuwa wanasafiri umbali mrefu yapata kilomita 10,20,30 ,100 hadi 200 kufuata huduma za afya katika kituo cha afya,zahanati au hospitali ya wilaya ambapo hali hiyo ilikuwa inapelekea akina mama wajawazito kutopata huduma nzuri za ujauzito kwa sababu ya umbali lakini pia kujifungulia majumbani kwa sababu huduma za zahanati na vituo vya afya zilikuwa mbali sana na hivyo ilikuwa ngumu sana wakipata hitaji lakuleta mtoto duniani kufika umbali huo na kupata huduma hospitali.
“Matokeo yake akina mama wengi walijifungulia majumbani au kwa wakunga wa jadi ambapo watoto wengi wachanga walikuwa wanafariki lakini wengine walikuwa wanazaliwa na matatizo ya mtindio wa ubongo kwa sababu ya kukosa huduma ya afyua wakati wa kujifungua.
Hata hivyo anasema katika kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto ,kwa watoto wenye umri wa miaka mitano na mama mjamzito ambapo kipaumbele ilikuwa ni kujenga vituo vya huduma karibu na wananchi kwa kujenga zahanati ambapo katika kipindi cha miaka mitatu, zaidi ya zahanati mpya 1,200 zimejengwa kwenye vijiji na kusogeza huduma karibu na wananchi lakini pia vituo vya afya zaidi ya 800 vimejengwa ambavyo vina uwezo wa kulaza,kufanya upasuaji wa akina mama wajawazito lakini pia kutoa huduma ya watoto wachanga na malezi ya watoto lakini pia kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi wengine.
“Kwa hiyo vituo hivi vya afya ambavyo vimejengwa vimepunguza sana ile ‘gape’ ya wananchi kufuata huduma mbali na mazingira yao na haya tunasema ni mafanikio ,lakini pia tumeendelea kujenga hospitali za halmashauri ambazo kila halmashauri sasa imejengewa hospitali ambayo inakuwa sasa ni hospitali ya rufaa ndani ya halmashauri ambapo wagonjwa wanaanzia ngazi ya zahanati,kituo cha afya hadi ngazi ya halmashauri .
Anasema ,uwekezaji katika miundombinu hii imeboresha sana upatikanaji wa huduma za afya kwa watoto wachanga,akina mama wajawazito lakini pia na watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wananchi kwa ujumla.
Anasema hatua hiyo imepelekea kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa zaidi ya asilimia 35 lakini imepunguza sana vifo vya watoto chini ya miaka mitano na kwa kiasi kikubwa sana tumepunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka vifo 556 mwaka 2016 mpaka vifo 104 kati ya vizazi hai 100,000 mwaka jana 2023.
Aidha anasema vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vimepungua kwa asilimia 36 kutoka Vifo kutoka Vifo 67 mwaka 2016 Kwa vizazi hai 1,000 Hadi kufikia Vifo 43 Kwa kila vizazi hai 1,000 huku akisema kwa watoto wachanga vimepungua kwa asilimia 4 tu kutoka Vifo 25 Kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2016 hadi vifo 24 Kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022 ambayo sawa na kupungua Vifo vya watoto wachanga 2,400 Kwa mwaka.
(chanzo TDHS 2022)
“Kwa hiyo kwa ujumla,tumepunguza sana vifo vya watoto wachanga,vifo vya watoto chini ya miaka mitano,na vifo vya akina mma wajawazito,na hii ina maana kwamba watoto wetu sasa wanapata huduma bora za afya tangu wakati mama ni mjamzito anaendelea kulea ujauzito kwa kwenda kliniki na tumeweka viwango kwamba angalau mama ahudhurie kliniki siyo chini ya mara nne mpaka anajifungua.
Aidha anasema hivi sasa zaidi ya asilimia 80 akina wajawazito sasa wanafika kwenye kliniki,wanahudhuria mahudhurio yote manne na wanajifungua kwenye vituo zaidi ya asilimia 90.
“Kwa hiyo tumeona hii ni hatua nzuri sana katika malezi na makuzi ya mtoto hasa katika kuboresha afya ya mtoto na afya ya mama .”anasisistiza Dkt.Dugange
Naibu Waziri huyo anasema katika kipindi cha kuanzia 2021, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 900 kwa ajili ya unuzi wa vifaa tiba ambavyo vimenunuliwa kwenye ngazi ya zahanati ambapo vituo vya afya sasa vinafanya upasuaji na ngazi ya hospitali za halmashauri .
Anasema katika mwaka 2023/24 Rais ametoa zaidi ya shilingi bilioni 125 ambapo halmashauri zote 184 zimepata fedha siyo chini ya milioni 700 huku nyingine zikipata shilingi bilioni moja hadi 1.5 kulingana na mahitaji.
Anasema “hatua hiyo imefanyika ili kutoa huduma bora kwa watoto wachanga,walio chini ya umri wa miaka mitano,akina mama wajawazito na wananchi wengine kwa ujumla.”
Vile vile anasema,magari ya wagonjwa zaidi ya 500 yamenunuliwa na yamepelekwa katika kila jimbo ambapo kuna majimbo yamepata magari zaidi ya mawili lakini na magari ya usimamizi.
“Tunapoongelea afya bora kwa watoto wetu ni pamoja na kupata chanjo ,kwa hiyo watoto wetu hawa wanahitaji chanjo na ufuatiliaji .
Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inayotekelezwa,inalenga kuongeza kasi ya mafanikio yanayopatikana katika huduma za Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ili watoto wote wenye umri wa kuanzia 0 hadi miaka minane waweze kufikia hatua zao timilifu za ukuaji kwa maslahi mapana ya watoto wenyewe,jamii na Taifa kwa ujumla.
Japhet Mwangai mkazi wa Mji Mpya jijini Dodoma anaiomba Serikali iendelee kuongeza jitihada hasa katika kupunguza vifo vya watoto kwani idadi ya wanaokufa kwa sababu mbalimbali bado ni kubwa.
Mtaalam wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Davs Gisuka anasema jitihada zianzofanywa na serikali katika kujenga,kuboresha vituo vya afya,zahanati na hospitali zina mchango mkubwa katika ukuaji wa mtoto.
“Moja ya maeneo makuu matano ya kihunzi cha Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) ni Afya,na ili mtoto akue na kufikia utimilifu wake anahitaji kupewa mahitaji ya msingi ambapo afya ni hitaji mojawapo linalohitajika ,
“Mtoto mwenye afya bora huwa na makuzi bora ya ubongo na akili”anasema Davis
More Stories
Mfumo unavyokwamisha wanawake kuwa viongozi
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi