October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wauguzi na Wakunga Watakiwa Kutumia Utaalamu wao kwa ajili ya Ustawi wa Taifa

Na Mwandishi wetu ,TimesMajira ,Online,Dodoma

WAUGUZI  na Wakunga nchini wametakiwa kutoa huduma kwa kuzingatia miongozo iliyopo wakati wakitoa huduma kwa weledi ili kufikia malengo na matumaini ya wateja kwa ajili ya ustawi wa Taifa.

Rai hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu ya Afya,Edward Mbanga wakati wa ufunguzi wa  kikao kazi  cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi wauguzi wakuu wa wilaya kinachofanyika jijini Dodoma.

Mbanga amesema  kuwa wauguzi na wakunga ndio watendaji wakuu katika vituo vya afya kwenye ngazi ya jamii hadi Taifa hivyo uwajibikaji mzuri na utawala bora utaboresha utendaji kazi wao .

“Viongozi mnatakiwa kuwa wabunifu, wachapa kazi, wenye nidhamu na mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa majukumu yenu,kwahiyo  ni lazima msimamie utoaji wa huduma uliyo mzuri na wenye heshima na utu.”amesema

Aidha, Amewakumbusha  washiriki hao kuwa, suala la huduma za uuguzi na ukunga ni suala la  ubinadamu zaidi na kuvaa viatu vya wagonjwa wao.

“Hakuna aliyegongwa muhuri wa kuugua  au kuwa mgonjwa akalazwa ,sisi sote ni wagonjwa watarajiwa kwahiyo kama ambavyo sisi tungependa kuuguzwa vizuri, kijibiwa kwa kauli nzuri basi tuhakikishe tunasimamia maadili ya kazi,”amesema Mbanga

Hatahivyo amesema kuwa, Serikali inawahakikishia itaendelea kufanya kazi pamoja na waauguzi  kwa kutoa miongozo thabiti na kuhakikisha upatikanaji wa nyenzo muhimu katika hospitali na vituo vya kutolea huduma ya afya na kuboresha mazingira ya kazi yaliyo bora na salama.

Amesema kuwa, hivi karibuni kumekuwa na malalamko  mbalimbali ya kiutendaji  na kitaaluma kutoka kwa wateja  wanaofika kupata huduma za afya na hivyo kuleta taswira mbaya  kwa taaluma yao na kuonyesha hakuna usimamizi mzuri wa utoaji huduma za uuguzi na ukunga.

“Tungependa  wateja wetu watoe sifa  badala ya malalamiko hivyo kikao hiki mje na mipango ya kuondokana na malalamiko kwani taaluma yenu ni zaidi taaluma.”