September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo aanza ziara kutatua kero za wananchi

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Ilala, kuwa Serikali ya awamu ya sita itahakikisha kero zote zinazogusa wananchi zitatatuliwa ndani ya muda mfupi kwanzia sasa.

DC Mpogolo ameyasema hayo Septemba 10, 2024 kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wananchi kutoka Kata ya Zingiziwa, Msongola,Chanika na Buyuni.

Akizungumza na wananchi katika mkutano  huo, Mpogoli amesema, Serikali inautaratibu wa kufanya mikutano ya kusikiliza na kutatua  kero za wananchi, ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati ili kuweza kuendelea kuleta maendeleo nchini.

Ikiwa ni mkutano wa kwanza wa ziara hiyo, wananchi wa kata hizo walipata nafasi ya kuwasilisha kero zao zinazohusu Sekta mbalimbali afya, elimu, umeme, miundombinu ya barabara, masoko, ardhi, uchumi na ajira katika sekta binafsi.

Ambapo kati ya kero hizo ilikuwa ni pamoja na uwepo wa mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Ilala na Wilaya ya kisarawe ambao umekua kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Ilala.

Aidha akijibu kero zinazohusu elimu hasa michango ya mitihani kila wiki Mpogolo, amewataka walimu kufuata utaratibu na kukemea michango isiyopitia katika kamati za shule, huku akiwataka wazazi kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula shuleni.

Kero nyingine iliyotolewa majibu ni juu ya miundombinu ya barabara korofi ambapo wananchi wamehakikishiwa kutengeneza hivi karibuni kupitia mradi wa DMDP awamu ya pili ambao ni mkombozi kwa barabara zote zilizopo katika mradi pamoja na kuahidi kushughulikia kero za ukatishwaji ruti za daladala zilizopewa kibali na Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri wa ardhini(LATRA)kufika zingiziwa na nzasa.

Pia Mpogolo, ametumia nafasi hiyo kuwatambulisha wanasheria watano wataokua wilayani hapo ili kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo ili waweze kupata haki zao.

Na kuwahimiza wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kujiandikisha katika daftari la wakazi ili wawe na sifa ya kupiga kura katika uchaguzi utaofanyika nchini.