November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CPA Makalla:Hatutawaletea wagombea wakusafishwa na dodoki

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Arusha

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Taifa,CPA Amos Makalla, amesema chama hicho hakipo tayari kusimamisha wagombea wa nafasi za uongozi wasiyokubalika na jamii.

Makalla amesema hayo leo,Septemba 7,2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shirika vilivyopo eneo la Mto wa Mbu.

Amesema, wapo viongozi ambao hawakubaliki katika jamii ikiwemo kutotatua kero za wananchi na kutosoma taarifa za mapato na matumizi.

“Niwaombe ndugu zangu muendelee kukiamini chama cha mapinduzi na kukipa kura nyingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na tunawaahidi kuwaletea wagombea wanaokubalika na wananchi na siyo mgombea mpaka umfafishe na dodoki sisi muda huo hatuna”,amesema Makalla.

Pia amewataka wananchi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la makazi Octoba 12 hadi 20 mwaka huu tayari kwa ajili ya kupiga kura.

“Tujitokeze kwa wingi ndani ya hizo siku 10 kwenda kujiandikisha kwenye daftari la makazi ili tuweze kushiriki kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwani kitambulisho pekee katika ucbaguzi huu hakitoshi”, ameongeza.

Aidha ameongeza kuwa,CCM kitahakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa amani, utulivu na haki, huku akisema kuwa matokea ya uchaguzi yatatangazwa kwa uwazi na haki.

“Mshindi atatangazwa kwa uwazi na atatangazwa atakaye kuwa na kura nyingi na si vinginevyo” amesema.