Daud Magesa na Judith Ferdinand,Timesmajira Online, Mwanza
Chama cha United Democratic Party (UDP),kimeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi daraja la J.P.Magufuli maarufu Kigongo-Busisi,ambalo linagharimu kiasi cha bilioni 716.33,ambao unatarajiwa kukamilika Desemba,2024.
MWENYEKITI wa Chama cha United Democratic Party (UDP),John Cheyo, Agosti 30,2024,aliongoza wanachama wa chama hicho, kutembelea mradi wa ujenzi wa daraja hilo la J.P.Magufuli,mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa mara baada ya kutembelea mradi huo,Cheyo amesema chama cha UDP,kimeridhishwa na kufurahishwa na maono ya Hayati John Magufuli ambayo yanatekelezwa na Rais Dkt.Samia kwa vitendo, ikiwemo daraja hilo ambalo likikamilika litaunganisha uchumi wa nchi na nchi jirani.
“Tunapotaka kuisaidia serikali ifanye vizuri si kupinga tu, tukaona twende kwenye mradi mmoja kuona kodi zetu zinafanya nini?.Daraja hili kazi imefanyika kwa fedha za Watanzania na wanajivunia fedha zao zimefanya kazi ya kutukuka,”amesema Cheyo.
Pia amesema, katika mradi huo wahandisi wazawa wameonesha umahiri na uwezo.”Hivyo baada ya daraja hilo kukamilika, tunaweza kuamua kujenga miradi mingine ya aina hiyo ya kuleta fedha bila kutegemea wahandisi wageni,”.
“Mwakani kuna uchaguzi mkuu,niwaambie wanaotaka kushindana na Dk.Samia kwa utekelezaji huu wa miradi ya kimkakati ukiwemo huu wa Daraja la J P.Magufuli,wajipange na wajiandae vizuri wana kazi,kwani ameiteka mioyo ya watu,”amesema.
Mwenyeketi wa UDP Mkoa wa Kagera,Majaliwa Yusufu,amesema serikali imefanya kazi nzuri ya kujenga daraja hilo, ambalo litaondoa changamoto iliyokuwepo ya kusubiri vivuko na kurahisisha usafiri na biashara.Hivyo amempongeza Rais Samia kwa kutekeleza maono ya mtangulizi wake.
Katibu Mwenezi wa UDP Mkoa wa Mwanza,Paulo Magilinga,amesema,walikuwa wakisumbuka wanapokosa kivuko.
“Magufuli alionesha uzalendo, na Rais Dkt.Samia ameendeleza maono hayo, kikubwa mkandarasi alipwe akamlishe daraja kwa wakati na katika uchaguzi wa mwakani wakati wa kampeni tutapita hapa,”amesema.
Aidha Katibu Mwenezi wa UDP Taifa,Erasto Nyaga amesema; “ UDP tumekuwa chama cha kwanza cha siasa kutembelea mradi wa Daraja la J P. Magufuli na wataendelea kwa mingine.
Awali msimamizi wa mradi huo kutoka TANROADS,Mhandisi Devotha Kafuku amesema, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 90.5,kupitia programu ya kuewaendeleza Watanzania wapo asilimia 93 ambapo mradi unatarajiwa kukamilika Desemba 2024.
“Daraja hili ni la kimkakati linaunganisha nchi ya Kenya,kuanzia Sirari kupitia Simiyu,Mwanza, Geita,Kagera na Kigoma.Pia litaunganisha nchi za Burundi, Rwanda,DRC na Uganda, litakuwa na njia mbili za kwenda na kurudi pamoja na njia ya za waenda kwa miguu,”amesema.
Mhandisi Kafuku amesema daraja kuu kiunganishi linajengwa kwa teknolojia ya kisasa,pia serikali imefanya uwekezaji kwa wataalamu wamepata ujuzi wa kutosha kujenga madaraja bila kutegemea wageni,huku changamoto ni vifaa.
Naye Mhandisi Aloyce Kadokado,amesema ujenzi wa daraja la J. P.Magufuli umetekelezwa kwa viwango kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya madaraja, lina nguzo tatu kuu ambapo zimebaki mita nane ili kuunganisha nguzo hizo kisha kumwaga lami.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba