October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mmoja wa wanafunzi Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kwa USO waliopata mshutuko na kupoteza fahamu akipatiwa huduma ya kwanza na mmoja wa watoa huduma za afya mara baada ya kutokea ajali ya moto katika moja ya bweni la shule hiyo usiku wa kuamkia jana. Na mpiga picha wetu.

Bweni lateketea kwa moto, wanafunzi wanusurika kifo

Na Mwandishi Wetu, Bukoba

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Kwa USO iliyopo Halmashauri ya Wilaya Bukoba Mkoani Kagera wamenusurika kifo baada ya bweni la shule hiyo kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana.

Wakizungumza tukio hilo jana mjini hapa baadhi ya wanafunzi walisema baada ya kuona bweni likiungua waliingiwa hofu.

Mmoja wa wanafunzi hao, Angel Mulokozi, amesema baada ya kuona tukio hilo la moto alipata mshutuko na kupoteza fahamu, lakini anashukuru Mungu wanafunzi wote wanaendelea vizuri.

“Tulikuwa darasani tukijisomea na baada ya kuona kinachoendelea nilipata mshutuko kwa kuwa nimeona kitu ambacho sikuwahi kukiona katika maisha yangu ila kwa sasa namshukuru Mungu naendelea vizuri na wanafunzi wote waliopata mshutuko kama mimi tunaendelea vizuri,” amesema Angel.

Kwa upande wake mlezi wa wanafunzi matroni katika shule hiyo ambaye ameongea kwa sharti la kutotaka jina lake litajwe amesema alikuwa kwenye moja ya bweni ambalo limetazamana na bweni lililouungua alihamaki baada ya kuona moto umeshakuwa mkubwa licha ya jitihada ya kuzima moto ilishindikana kutokana na uwezo wa wanafunzi.

“Nilikuwa kwenye bweni langu nikasikia kelele na nilipotoka nje ndipo nilipoona bweni la wasichana likiungua ambalo ni la ghorofa, wanafunzi walianza jitihada za kuzima moto huo, lakini nguvu ya moto ilituzidi japo tulijitaidi kuokoa mali za wanafunzi zilizokuwa kwenye bweni la chini, maana bweni lililokuwa linaungua ni la ghorofa, tumebahatika kutoa vitu vya wanafunzi kwenye bweni la chini na kutokana na kuungua kwa mali za wanafunzi ndo wengine wakaanza kuzimia lakini sasa wanaendelea vizuri.” amesema

Matroni huyo aliongeza kuwa wapo wanafunzi ambao walikimbizwa hospitalini na wengine walipata huduma palepale baada ya magari ya huduma za kwanza kuwasili kwenye eneo la tukio.

Kwa upande wake mkaguzi Msaidizi wa Polisi na Kaimu Kkuu wa Upelelezi Bukoba, Franck Sambaa ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo walifika kwenye eneo la tukio kwa kushirikiana na jeshi la zima moto na uokoaji ili kuhakikisha madhara zaidi hayatokei.