November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa soka wafikiwa na mfumo wa NeST

Ally Kamwe Ahmad Ally kutangaza mfumo wa NeST kwenye soka

Na Joyce Kasiki,Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti na Ununuzi wa umma (PPRA) inatumia jukwaa la mpira wa  soka kutangaza mfumo mpya wa kielektroniki wa ununuzi wa umma na Kongamano la Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki  kupitia Meneja Mawasiliano wa timu ya soka ya Klabu ya Yanga Ally Kamwe kama Balozi wa mfumo huo.
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Sept 9-12 mwaka huu ambapo nchi nane za Afrika Mashariki zitashiriki Kongamano hilo huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pamoja na mambo mengine atauzindua rasmi mfumo huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Denis Simba amesema kuna fursa kubwa kwenye michezo kupitia tenda za Serikali ambazo zipo kwenye Mfumo wa NeST huku akimwomba Kamwe kufikisha salamu hizo pia kwa msemaji wa Klabu ya soka ya Simba Ahmed Ally ili washirikiane kusambaza ujumbe huo ili wadau wa soka wamejisajili kwenye mfumo na wapate fursa za zabuni za Serikali zinazohusiana na masuala ya michezo.
“Kwa mfano Mzabuni anayejenga Uwanja wa Mpira wa Miguu jijini Arusha utakaotumika kwenye michuano ya AFCON 2027(Samia Stadium),amepatikana kupitia Mfumo wa NeST. Ujenzi huo unagharimu zaidi ya Sh. Bilioni 286 na utatoa ajira nyingi kwa watanzania.”amesema Simba
Aidha amesema, Vivyo hivyo,kwa ukarabati na ujenzi wa viwanja vya Serikali, PPRA PPRA inafuatilia upatikanaji wa wazabuni hadi utekelezaji wa mikataba yake.
“Zipo zabuni nyingi za usambazaji wa vifaa vya michezo kwenye taasisi za umma , hizo zote sasa zinatolewa kupitia Mfumo wa NeST ambao PPRA tunausimamia. Lakini pia,wanamichezo tunapaswa kuwaeleza kuwa wana fursa ya kushiriki hizi tenda. “
Ameongeza kuwa “Leo tunakupa rasmi jukumu la kuwakaribisha watanzania na wadau wa ununuzi wa umma kushiriki Uzinduzi wa Mfumo wa NeST, Septemba 9-12, 2024, jijini Arusha. Wajisajili kupitia tsms.ppra.go.tz wajisajili kwenye Mfumo wa NeST kupata tenda za Serikali kupitia nest.go.tz, Nifikishie salamu zangu kwa ndugu yetu Ahmed Ally na wengine. Tumeanza na wewe, tunahitaji mchango wao pia, tutawafikia.
Kwa upande wake Ally Kamwe amesema mambo ya tenda za serikali yamekuwa yakizungumzwa tofauti kwamba kupata tenda hizo lazima mtu awe na  ‘connection ‘ huku akisema sasa hivi connection ni mfumo wa NeST.
Amesema,mfumo huo sasa unakwenda kupunguza janjajanja katika upatikanaji wa tenda hizo na hivyo kuunga mkono jitihada za Serikali za Rais Samia Suluhu Hassan za kupeleka maendeleo ya wananchi kwa kasi.
xxx