November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shamrashamra maadhimisho ya miaka 60 JWTZ yaendelea

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira


SHAMRASHAMRA za maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zinaendelea baada ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA kufungua mashindani ya utamaduni ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF).

Mashindano hayo yameanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka huu na CDF, Jenerali John Mkunda yakishirikishwa bendi za muziki 10 na vikundi vya Ngoma na Utamaduni Tisa vyote kutoka JWTZ.


Akifungua mashindano hayo juzi jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mwinjuma alisema, anampongeza CDF kwa kuanzisha mashindano hayo kwamba amefanyia kazi maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu kuendeleza sanaa ya utamaduni na kuulinda.


“Tunasahau sisi ni nani, tunasahau utamaduni wetu, nampongeza sana CDF kwa kulifanyia kazi hili na kurudisha sanaa na utamaduni wetu ni sehemu ya kuulinda usipotee”amesema Naibu Waziri Mwinjuma.


Mwenyekiti wa Kamati Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano hayo, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, lengo la CDF ni kurejesha sanaa ya utamaduni ikiwa ni sehemu ya kuelimisha vijana na kuwakumbusha asili ya Watanzania.

Amevitaja vikundi hivyo kuwa ni, Nyuki Jazz Bendi (kutoka Zanzibar), Mlale Jazz Bendi, Mwenge Jazz Bendi, Air Jazz Bendi maarufu kama wanaangaanga, JKT Kimbunga, Ruvu Stars, Mbweni Jazz Bendi maarufu kama Wazee wa Jodari, Mkutopora Jazz Bendi ama Matajiri wa Zabibu, Mpwapwa Jazz Bendi na TMA Jazz Bendi.


Mwenyekiti Mkaremy amevitaja ViKundi vya Ngoma kuwa ni, Nyuki Cutural Troup kutoka Zanzibar, Mgulani JKT, Makutopola JKT, Mwenge Sauti ya Umoja, Orijoro Sanaa, Mlale JKT Sanaa, Mbweni JKT na Mpwapwa.

Kwa upande wake,Mkuu wa Utumishi JWTZ, Meja Jenerali, Marco Gaguti, amesema katika madhimisho ya mwaka huu jeshi hilo liko tayari kukuza utamaduni, sanaa na michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Michezo.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Dk. Kedmom Mapana amesema sanaa na utamaduni si burudani bali ni biashara baraza lake linawakaribisha wanaotaka kuwekeza katika tasnia hiyo wakati ni sasa.