November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mashudu ya alizeti yapata soko China, wakulima watakiwa kuchangamkia fursa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wakulima wa zao la alizeti pamoja na mazao mengine yakiwemo tumbaku, pilipili na parachichi wamehakikishiwa uwepo wa masoko ya mazao nchini China huku Serikali ikiendelea na juhudi za kufufua masoko katika nchi nyingine Duniani.

Akizungumza tarehe 14 Agosti,2024 mara baada ya kutia saini Hati ya Makubaliano ya Mauziano ya Mashudu ya Alizeti nchini China, iliyosainiwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (Mb) pamoja na Waziri wa Mamlaka ya Forodha ya Watu wa China, Mhe. Yu Jianhua katika Ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dar Es Salaam, Mhe. Silinde amesema kuwa “makubaliano hayo yataongeza soko la zao la Alizeti hapa nchini.” Ameeleza kuwa soko la Alizeti linapanda kwani baada ya kukamua mafuta wakulima na wafanyabiashara watapata mashudu ya kuyasafirisha kwenda China.

Mhe. Silinde ameongeza kuwa wamepata fursa ya mazungumzo ambapo nchi ya China imekubali makampuni takribani tisa kutoka Tanzania yanayoruhusiwa kusafirisha zao la parachichi, kusafirisha zao ambapo Tanzania itasafirisha bidhaa zake moja kwa moja kwenda China bila kumlazimu mkulima au mfanyabiashara kusafirisha kupitia nchi zajirani kama ilivyokua hapo awali.

“Cha mwisho kuna baadhi ya makubaliano ambayo bado yako katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika Serikali zote mbili. Mhe. Yu Jianhua amenithibitishia kwamba watatuma timu yao kuja kuharakisha sehemu za makubaliano ikiwemo upelekaji wa pilipili nchini China zinakamilika; ikiwa ni pamoja kuongeza usafirishaji wa zao la tumbaku nchini humo,” amehitimisha Mhe. Silinde.