November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Abdul apandishwa kizimbani akikabiliwa na mashtaka sita ya ubakaji,ulawiti

Na Ashura Jumapili ,TimesMajira online Kagera,

Abdul Seleman ( 30 ),mkazi wa Kata ya Kahororo Tarafa ya Rwamishenye mkoani Kagera,amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba akikabiliwa na mashtaka 6 ya ubakaji na ulawiti watoto 4 wa shule ya msingi.

Akiongea na waandishi wa habari Agosti 14,2024,Wakili wa Serikali Agness Owino,amesema mshitakiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Endrew Kabuka wa Mahakama ya Bukoba na kusomewa mashtaka yanayomkabili katika kesi namba 22889 ya ubakaji na kulawiti ya mwaka 2024,hata hivyo mshtakiwa alikana mashtaka hayo.

Owino amesema mshitakiwa alitenda makosa hayo tarehe tofauti kati ya mwezi wa nne(Aprili) hadi wa saba(Julai)mwaka huu, kwa watoto hao wenye umri kati ya miaka ( 7- 9 )ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi.

Amesema mshitakiwa anakabiliwa na mashitaka 6 ambapo mashitaka 4 ya kubaka kinyume na kifungu 130 (1 ),(2 ), kifungu cha kanuni ya adhabu 131 (1)sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022,makosa 2 ya kulawiti kifungu 134 (1) ,(2 ) sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Pia ameeleza kuwa upelelezi umekamilika na hoja za awali zimesomwa na mashahidi wameanza kutoa ushahidi kesi inaendelea itasikilizwa tena leo Agosti 15,2024, majira ya saa tatu asubuhi.

Wakati huohuo mshitakiwa huyo Abdul Seleman ,amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Bukoba kwa kesi ya kubaka mtoto mwenye umri wa miaka ( 9 ) mwanafunzi wa darasa la tatu kesi ya ubakaji namba 22890 ya mwaka 2024.

Akiongea na waandishi wa habari Wakili wa Serikali Everester Kimaro,amesema mshitakiwa amesomewa shitaka moja la ubakaji mbele ya Hakimu Frola Kaijage wa Mahakama ya Wilaya ya Bukoba na mshitakiwa amekana shitaka.

Wakili kimaro,amesema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na shahidi ametoa ushahidi wake mbele ya mahakama hiyo.

Amesema mtoto aliyebakwa hakumbuki tarehe aliyofanyiwa ukatili huo lakini tukio lilifanyikia Kata ya Kashai Manispa ya Bukoba.