September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Siku 6 za ziara ya Rais Dkt. Samia Morogoro zilivyoacha alama ya kuchochea maendeleo

Na MwandishiWetu,Timesmajiraonline,Moro

AGOSTI 7 , mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara ya siku sita mkoani Morogoro. Ziara hiyo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na wananchi wengi wa mkoa huo.

Kile ambacho wananchi walikuta wakitamani kuona na kusikia kutoka kwa Rais Samia, wamekishudia kwa macho yako na sasa kila mmoja ana shauku ya kuona Morogoro inavyopaa kwa maendeleo.

Katika ziara hiyo Rais Samia alitoa maelekezo mbalimbali ambayo yanalenga kuchochea maendeleo ya wananchi na kutatua kero zinazowakabili.

Miongoni mwa maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia ni pamoja na ya kujengwa hospitali ya rufaa na kufufuliwa viwanda.

Kwenye mkutano wake wa Agosti 6, 2024 uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Rais Samia amemuelekeza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutafuta sh. bilioni 5 ili kuanza ujenzi wa hospitali ya rufaa.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo kutokana na ombi la Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, aliyeeleza hospitali ya rufaa ya mkoa imezidiwa nguvu.

“Hospitali tuliyonayo imezidiwa nguvu, tunaomba tupate hospitali nyingine ambayo itawezesha kuwahudumia wananchi wa Morogoro na kutoka maeneo mengine ya jirani, kuipunguzia mzigo hospitali iliyopo,” alisema Abood.

Kuhusu ombi hilo, Rais Samia amekiri kuwa hospitali hiyo haina hadhi ya kuitwa hospitali ya rufaa, hivyo ni lazima Serikali iingilie kati na kujenga nyingine. “Kwa kweli hospitali iliyopo haikidhi vigezo kuitwa hospitali ya rufaa kwa ulimwengu wa leo.

Nimempa Waziri wa Afya atafute angalau bilioni tano za kuanzia tuanze ujenzi wa hospitali ya rufaa kwa kuanzia majengo yatakayotoa huduma za mama na mtoto kabla ya kwenda kwenye huduma nyingine,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alieleza mpango wa Serikali wa kuurudishia hadhi Mkoa wa Morogoro kwa kuvifufua viwanda vilivyokuwepo awali kwa kuanzia na kiwanda cha vipuri kilichopo Mang’ula.

“Wanaojua historia ya Morogoro wanaelewa nafasi ya viwanda. Tunataka kurejesha ile hadhi ya Morogoro ya viwanda, tunataka Morogoro ikashindane na Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.

Tayari nimeshampa maelekezo Waziri wa Viwanda, Dkt. Selemani Jafo kuhakikisha viwanda vilivyopo havifi na vilivyokufa vifufuliwe hata kama havitazalisha yale mazao ya awali basi vizalishe vitu vingine.

Alisema hatua hiyo inalenga kuzalisha ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa Mkoa wa Morogoro ambao kwa sasa una fursa nyingi za kiuchumi zinazopaswa kuchangamkiwa. Katika hilo, Rais Samia amewataka viongozi wa mkoa huo kuacha kuvutana, badala yake kutenga maeneo ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wanaotaka kuwekeza mkoani humo.

“Uwepo wa reli na umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unafanya mkoa huu kuwa sehemu nzuri ya uwekezaji. Reli zote mbili ile ya MGR na SGR zote zinapita kwenye mkoa huu.

Nasaha zangu kwenu acheni mivutano, tengeni maeneo ya uwekezaji ili wawekezaji wakifika wakute maeneo waweke fedha zao uwekezaji uendelee,” ameagiza Rais Samia. “Kwenye elimu tumejenga Chuo cha Veta katika kila wilaya, lengo vijana wajifunze kulingana na amali zilizopo kwenye maeneo yao, sasa kwa kuwa tumeamua kuifufua sekta ya viwanda katika Mkoa wa Morogoro ni imani yangu kwamba vyuo hivi vitazalisha nguvu kazi itakayotumika kwenye hivyo viwanda. Wito wangu itumieni vyema fursa hii vijana wakasome,” alisema.

Katika ziara hiyo, Rais Samia hakukubaliana na ombi la kuufanya mkoa huo kuwa jiji akieleza bado haujakidhi vigezo vya kufikia hatua hiyo. Ombi hilo liliwasilishwa na mbunge wa Viti Maalumu kutoka mkoa huo, Dkt. Christine Ishengoma ambaye alieleza tayari mkoa huo una vigezo vyote vya kuufanya kuwa jiji.

Katika majibu yake, Rais Samia alisema kwa vipimo tulivyoviweka bado Morogoro kuwa jiji, kuna kazi kubwa inatakiwa kuendelea kufanyika na Waziri wa Tamisemi atasema kazi gani ifanyike ili Morogoro iweze kuwa jiji kwa sasa bado, hivyo timizeni wajibu wenu Serikali ije kutimiza wajibu wake.”

Akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha sigara cha Serengeti (Mkwawa leaf) aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Alisema kiwanda hicho kinapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhifadhi mazingira. Amesema hayo baada ya kutembelea mabanda mbalimbali kwenye kiwanda hicho na moja lilionyesha miti ikiashiria ni mapori ya kuni.

“Nimeona katika maonesho yenu kuna banda lina vimiti miti, lengo lilikuwa kuwarahisishia Watanzania hasa wanawake, kuwa mapori haya mnayopanda ya kuni, tupande kwa wingi.

“Hata hivyo, hivi sasa Watanzania tuna ajenda ya nishati safi ya kupikia, kuni bado siyo nishati safi, tunataka mpande misitu ile lakini tunaomba mtuunge mkono kwenye nishati safi ya kupikia,” alisema Rais Samia.

Akizungumzia umuhimu wa kiwanda hicho, Rais Samia alisema, “Nimeambiwa kiwanda kina wafanyakazi si chini ya 7,000, hiki cha tumbaku na kile cha kutengeneza sigara kikikamilika kitakuwa na wafanyakazi 12,000,” alisema.

Rais Samia alisema awali kulikuwa na madaraja ya tumbaku na lile la mwisho halikununuliwa, lakini hivi sasa kiwanda hicho kinanunua kila kitu hivyo kumpa faida mkulima.

“Kuanzia jani la tumbaku hadi kiungio cha jani, hakuna kinachotupwa kila kitu kwenye zao la tumbaku ni mali, hii inamuongezea mkulima faida,” alisema.

Rais Samia amezungumzia mpango wa Serikali wa bima ya afya kwa wote, akiomba kiwanda hicho kuunga mkono juhudi hizo ili wale watakaomwa vifua waweze kupata matibabu.

“Nimeambiwa kiwanda kimepanua uzalishaji na usafirishaji wa mazao, asilimia tano tu ndiyo itakayovutwa hapa nchini na inayobaki itakwenda nje, hivyo ile tano itakayovutwa hapa itakuwa na athari kidogo. Tunatarajia kiwanda kitatuunga mkono kwenye mpango wa bima ya afya ili wale watakaokuja na vifua na kukohoa wapate matibabu,” alisema.

Aidha Rais Samia alihitimisha ziara yake kwa kuzindua kiwanda Mkulanzi, akioa maelekezo ya kuhakikisha tatizo la sukari nchini linabaki historia kwa kukitaka kiwanda hicho kuzalisha kwa ajili ya wananchi hata kama kukiwepo kwa mabadiliko ya kisera, kikodi au mabadiliko yoyote.

Pia aliitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuingiza sukari kama moja ya chakula cha kuhifadhi, ili kukiwa na upungufu wa sukari nchini iweze kudhibiti upungufu, kwa kutumia akiba hiyo.

Rais Samia alisema hata kukiwepo kwa mabadiliko hayo kiwanda hicho hakitaweza kusitisha kuzalisha, hivyo kufanya uzalishaji ajili ya nchi.

Alisema uwepo wa kiwanda hicho kuna umuhimu wake katika uwekezaji kwa Serikali na sekta binafsi (PPP) katika kutoa uhakika wa kutoa sukari nchini.

Rais Samia alisema kiwanda hicho kimejengwa na taasisi za Serikali, hivyo kukiwa na mabadiliko mbalimbali uenda kwa sekta binafsi wasiridhike nayo na kuvuta nyuma kidogo, na uzalishaji ukapungua, lakini kiwanda hiki kitazalisha kwa ajili ya nchi.

”Niwaambie wana miradi, wanahisa tutaangalia iwezekanavyo kufanya utanuzi wa kiwanda hiki…nilipata tetemeko kidogo wa sukari kwa mwezi Februali au Machi hadi Aprili, ziliponyesha mvua nyingi viwanda havikuweza kuzalisha, lakini sukari kwenye baadhi ya maeneo ilikuwepo na baadhi ya maghala ilikuwepo, lakini watu wakabana na sukari ikapanda bei kupindukia, kiasi ambacho Mtanzania wa kawaida hasingeweza kununua.

”Sukari si chakula chetu wakubwa, ni chakula cha watoto, sisi wakubwa ikifika umri unakataa sukari na hata kama unatumia ni kidogo sana ila watoto hawawezi kuacha kutumia sukari ,lakini pia wafanyabishara wadogo wadogo kama mama lishe matumizi ya sukari ni makubwa unapomwambia akanunue sukari kwa sh. 7000 au 8,000 hawezi kupata chochote,”alisema.

Alisema uwepo wa kiwanda hicho kitaepukana na changamoto aidha za kumenyesha mvua, kwani akiba itakuwa ndani katika ghala ambapo itachukuliwa na kuwafikishia wananchi bila migogoro yoyote na heshima kuwepo.’

‘Kwa mtu binafsi huwezi kumwambia hatoe sukari ghalani labda uende na mtutu wa binduki na hapo kutakuwa hakuna utawala bora,”alisema.

Alisema aliwaambia watu wa NFRA waingize sukari kama moja ya chakula cha kuhifadhi, ambapo huko mbele watafanya NFRA kununua sukari na kuweka vile inavyotakiwa kuhifadhika ili inapotokea ukosefu wa sukari NFRA watakuwa nayo na kiwandani pia watakuwa nayo, hii tunaenda kuwahudumia wananchi bila kuwa na changamoto yoyote,” alisema.

”Nawapongeza kwa ajira mlizotengeneza kiwandani na mashambani hizi ni ajira nyingi, niombe muende nao vizuri hatutaki kuona vyama vya wafanyakazi wanakuja na kuleta matatizo kwa sababu kiwanda cha Serikali mambo yote yaende murua,”alisema .

Aidha, Rais Samia alisema kiwanda hicho kinatakiwa kuwa endelevu na kuondokana na dhana ya kitu kikiwa cha Serikali au kikiwa na mkono wa Serikali umakini wake unakuwa sio mkubwa.

Alisema hali hiyo imesababisha viwanda vingi vya Serikali kushindwa kuendelea. ”Nadhani kuna mambo ambayo Serikali inadhibiti viwanda hivi au kuna mambo tu kitu kikiitwa cha serikiali kinakuwa hivi,Meneja mradi nataka usimamie kwelikweli mradi huu.

Nataka uwe endelevu mradi huu, kama kutakuwa kuna mkono wowote unatoka juu kuingiza, zipo sera ya kiwanda nenda moja kwa moja sikwambii usiwe flexible, ila kiwanda hiki kisimame,” alisema na kuongeza;

”Sasa hapa natumia njia ya Rais wa Ethiopia, alikuwa akiwaambia huu mradi ukifa na wewe ufe, na mimi nasema mradi huu ukifa ufe nao, usife mradi wewe ukawa hai , mradi ukifa na wewe ufe , vinginevyo ukiishi na wewe uishi kwa manufaa ya taifa.”