Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
CHAMA Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) kimeomba serikali kuwabadilishia Muundo wa Utumishi wafanyakazi wasio wanataaluma (wasio walimu) ili kuwaongezea molari wa kazi.
Wametoa ombi hilo katika Kikao Maalumu cha siku moja kilichofanyika katika Ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi Mjini Tabora juzi baina ya THTU na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuratibu Maoni ya Wafanyakazi, Waendeshaji na Mafundi wa Vyuo Vikuu vya Umma nchini juu ya muundo uliohuishwa, Sarakiel Chaula amesema kuwa mapendekezo yao yanahusiana na muundo wa mishahara.
Amebainisha kuwa muundo wa mishahara wa PGSS ulioainishwa katika waraka namba 6 wa mwaka 2015 kwa watumishi wasio wanataaluma una maslahi madogo tofauti na muundo wa wanataaluma wasaidizi wa PUSS.
Amefafanua kuwa utofauti mkubwa uliopo kwenye muundo wa mishahara ya wafanyakazi waendeshaji wa taasisi hizo unawavunja moyo kwani hata kama una elimu sawa na mwanataaluma bado unalipwa mshahara mdogo.
‘Tunapendekeza watumishi wasio wanataaluma nao waingizwe katika muundo wa PUSS unaotumiwa na Wasaidizi wa Wanataaluma ili kupunguza pengo lililopo sasa la mishahara kwa watumishi wa taasisi za elimu ya juu nchini’, amesema.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) Paul Loisulie amesema kuwa muundo wa sasa wa mishahara ya wafanyakazi waendeshaji (wahasibu, utawala, masijala na wengineo) unawaumiza.
Amebainisha kuwa kupitia muundo huo watumishi hawa ambao ndio wengi zaidi wanajiona wanyonge licha ya kufanya kazi kwa masaa mengi na wakati mwingine wanatamani kuhamia kwenye taasisi zingine tofauti na za wanataaluma.
‘Tunaiomba serikali iangalie namna ya kuboresha au kurekebisha muundo wa mishahara kwa wafanyakazi wa Vyuo vya Elimu ya Juu wasio wanataalauma, ili watakapostaafu wawe na maisha mazuri tofauti na hali ilivyo sasa’, amesema.
Aidha ameomba serikali ikubali kukaa meza moja na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wasio wanataluma, Waajiri na Utumishi ili kupokea mapendekezo yao yanayolenga kuboreshwa muundo wa mishahara yao.
Loisulie amefafanua kuwa walishaandika na kupeleka mapendekezo yao kwa Waziri, Katibu Mkuu Kiongozi na Ofisi ya Rais lakini hadi sasa kile wanachokitaka hakijatimia.
Akiongea katika mkutano huo Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Cha Ustawi wa Jamii DSM Salma Fundi amesema kuwa muundo huo ukirekebishwa utasaidia sana kupunguza malalamiko ya watumishi waendeshaji wa Vyuo vya Elimu ya Juu.
Ameomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo kwa kuwa watumishi wengi katika Taasisi hizo ni wanawake, na hali zao kiuchumi sio nzuri kutokana na mshahara mdogo wanaolipwa na mafao madogo baada ya kustaafu.
Mwakilishi wa Ofisi ya Rais Utumishi Baraka Kilagu amewashukuru Viongozi wa THTU kwa kuwaalika kushiriki kikao hicho na kubainisha kuwa wamewapa mapendekezo ya hatua zinazopaswa kufuatwa ili kufanikisha azma yao.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Viongozi wa THTU kutoka Taasisi zote za Elimu ya Juu za umma hapa nchini ambapo washiriki walipata fursa ya kujadiliana na kutoa mapendekezo ya muundo wenye tija kwa ustawi wa watumishi wa taasisi hizo
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa