October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala.

Nabii Joshua:Tutamuombea Rais kibali cha kushinda uchaguzi ili atimize ndoto yake njema kwa Taifa letu

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Morogoro

Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala amesema Agosti Mosi na 2, mwaka huu zitakuwa siku za kipekee kwa ajili ya kuliombea Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Sambamba na maombi maalum kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ili Mungu aweze kuwapa Watanzania wawakilishi wenye maono chanya kwa ajili ya kusaidia kuharakisha maendeleo wakiwemo madiwani, wawakilishi na wabunge.

“Ndiyo maana tarehe 1 na 2 tutakuwa na maombi maalum kwa ajili ya kuliombea Taifa, lakini kubwa sana tutamuombea Rais wetu, Dkt. John Magufuli kwa sababu tayari Mungu amezungumza na sisi kwamba tumuombee neema wakati huu mgumu, sasa tunamuombea Rais kwa sababu nchi hii sasa ipo kwenye dhamana yake, na yeye ndiye kiongozi mkuu bado kwa nchi yetu,ana nafasi kubwa sana ya kufanya uchaguzi huu kuwa wa amani, ana nafasi kubwa sana ya kuifanya Tanzania ya kesho iendee kuwa Tanzania ya amani kama tulivyo. Nafasi hii aliyonayo ukubwa wake unahitaji maombi ya watakatifu wa Mungu, kumuombea hekima, nguvu na uwezo.Tutamuombea Rais kibali cha kushinda uchaguzi ili atimize ndoto yake njema kwa Taifa letu.

“Lakini sisi manabii, hasa mimi ambaye Mungu amenipa maono ya kulibeba Taifa hili kwa maombi kwa muda mrefu, ninatafsri wazi kuwa, Rais Magufuli bado ni mteule wa Mungu na tunapaswa kumpa tena nafasi ya kumuombea kwa Mungu ili amalize kipindi chake cha miaka 10 ya kikatiba, kusudi ndani ya miaka 10 hii tuone kipi ambacho Mungu aliweka ndani yake kwa ajili ya Watanzania.

“Kwa hivyo nakusihi wewe Mtanzania uendelee kumuombee Rais Magufuli kwa agizo la Nabii na nina hakika Mungu atatushindia na tutavuka kwa ushindi mkubwa sana;

Nabii Joshua ameyasema hayo mjini Morogoro wakati akizungumzia juu ya mkutano huo mkubwa ambao unatarajiwa kufanyika katika makao makuu ya Huduma ya Sauti ya Uponyaji, Yespa, Kihonda mjini Morogoro.

“Lipo jambo ambalo Mungu ameniagiza kwamba mwezi huu wa nane tarehe 1 na 2,katika kituo chetu cha Sauti ya Uponyaji tutakutakuwa na mkutano mkubwa sana wa uponyaji. Mkutano huu utakuwa mkubwa sana kwa ajili ya uponyaji, Mungu amenipaka mafuta na amenipa karama ya miujiza,na wengi wanaoamini kupitia huduma hii huwa wanafanikiwa sana.

“Kama mnavyofuatilia kwa muda mrefu ni kwamba tuna shuhuda nyingi za miuujiza mikubwa sana ambazo Mungu amefanya, Mungu amefanya miujiza mikubwa kupitia maji ya uponyaji ambayo nilitoa, pia tutatoa maji tena. Maji haya yanatolewa bure, maji haya yameombewa, yana nguvu na ukiyapata utashuhudia miujiza mikubwa. Hakikisha kwamba tarehe 1 na 2, haukosi katika ibada hiyo kubwa ya uponyaji wa kiungu,”amefafanua Nabii Joshua.

Amesema, mkutano huo ni muhimu zaidi kwa ajili ya maombi ili ukuu wa Mungu ukaonekane wakati tunaelekea kuchagua viongozi wetu kwa maana ya madiwani, wabunge na Rais wetu.

“Ni wazi kwamba wagombea watatoka vyama mbalimbali, tuna wajibu wa kuwaombea ili nchi yetu ivuke salama kwenye eneo hili gumu sana katika uchaguzi.

“Rai yangu kwa watu wote ni kwamba, nitakuwa sijakutendea haki kama nitakualika kwenye maombezi na uponyaji,wakati unategemea nauli yako ya kuja katika mkutano upewe rushwa na mgombea udiwani au mbunge katika jimbo lako au kata yako.

“Rushwa ni laana, eneo lolote ambalo linazingirwa kwa rushwa, watu wanaishi kwa rushwa kwa hongo huwa ni watu waliolaaniwa, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, rushwa ya uchaguzi haiwezi kutuondolea umaskini, mtu yeyote unayeweza kumchagua kwa sababu amekuhonga. Tafsri yake ni kwamba unakuwa umeuza haki yako ya mafanikio, kwa hiyo kama Mungu alikusudia kukubariki, laana inakuwa tayari imefanikiwa kwako.

“Ninaweza kukumbusha jambo, unakumbuka kwa yule mtu wa Mungu, Esau. Yeye alichukua rushwa akadanganywa,akahongwa chakula akauza haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Kwa hiyo ninataka ujiadhari sana na maisha ya rushwa katika kipindi hiki cha uchaguzi, Mungu wangu akubariki akujalie neema na akupe uwezo wa kuomba na kumtegemea ili uchague kiongozi, tupate viongozi,wazuri, wema ambao wanaweza kutuletea maendeleo tunayotaka,”amefafanua Nabii Joshua.