Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,Julai 22,2024 amezindua uuzwaji wa tiketi za kuingilia katika Tamasha la Pamba Day na kuwataka mashabiki na wapenzi wa timu ya Pamba Jiji kuwahi mapema kununua tiketi hizo.
Kutakuwa na tiketi za sh.100,000 kwa jukwaa la V-VIP, Sh.50,000 kwa VIP,sh.10,000 na sh. 3000 mzunguko ambapo tayari zaidi ya tiketi 5,300 zimeshauzwa.
Akizindua uuzwaji wa tiketi hizo uwanja wa Nyamagana,uliofanyika sambamba na mkutano wa wadau wa kutoa maoni kuhusu timu ya Pamba Jiji,amesema tiketi hizo zitatumika kuingilia uwanjani kushuhudia tamasha hilo la aina yake kuwahi kufanyika mkoani humu.
Mtanda amesema tamasha la Pamba Day linatarajiwa kufanyika uwanja wa CCM Kirumba, Agosti 10 mwaka huu ambapo zimetengenezwa tiketi 25,000 na kuwataka mashabiki na wananchi kuwahi kununua tiketi kabla hazijaisha.
Amesema serikali ikishirikiana na uongozi wa Pamba Jiji imedhamiria kurejesha heshima ya Mwanza katika soka na furaha ya mashabiki wa timu hiyo almaarufu Tour Poissant Lindanda wa ndani na nje ya nchi waliyoikosa kwa zaidi ya miaka 23.
Mtanda amewashukuru wachezaji wa zamani waliopo na waliotangulia mbele za haki,bodi kwa usimamizi ulioiwezesha timu kuingia kambini kujiandaa kwa msimu na sasa ni wakati wa watu wenye maoni ya kuboresha timu wauone uongozi ili watoe maoni hayo.
“Kazi iliyobaki ni kumlea mtoto Pamba Jiji,wenye kuisadia na kushusha ni wana Mwanza wenyewe,wapo watakaozipokea timu pinzani na kufichua siri ya kambi ya timu,wanatamani kuona migororo wajinufaishe, siku za mechi kwenye msimu ujao watajitokeza watu kuwapokea wageni,” amesema na kuongeza;
“Tusiwe wa kwanza kushusha timu matamanio ya walio wengi na siyo matamanio ya wachache wanazipokea timu pinzani za nje ya Mkoa, hatutakubali mtu wa kuvuruga na hatutaoneana haya,kama noma na iwe noma,tuendelee kuiunga mkono Pamba Jiji,”.
Mtanda amesema Pamba Jiji ni mali ya wadau kila mmoja ana haki ya kuipgania hata kwa matambiko na maombi ili timu ifanye vizuri, hivyo waipe ushirikiano wa kutosha.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa timu hiyo imekamilika sababu usajili uliofanywa ni mzuri kutokana na mchujo wa wachezaji zaidi ya 900, pamoja na usajili wa wachezaji kutoka nje wapo wazawa katika kikosi hicho maarufu kama Wana Kawekamo.
Tamasha la siku ya Pamba (Pamba Day) litatumbuizwa na wasanii mbalimbali wanaotokana na Mkoa wa Mwanza wakiongozwa na Fid Q, Harmonize na wengine wengi.
More Stories
Wanafunzi 7176, kufanya mtihani wa taifaÂ
Mtendaji afukuzwa kazi kwa rushwa
Mwalimu aliyetuhumiwa kumbaka mwanafunzi wake atiwa mbaroni