November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watumishi wa ardhi,wenyeviti wa mitaa Ilemela waonywa

Na Daud Magesa, Timesmajira Online Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda amewataka watumishi wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,kutatua kero za ardhi na kuwahudumia wananchi kwa haki na kwa wakati ili kutochafua taswira ya CCM.


Pia amewanyoshea kidole baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa kuzalisha migogoro ya ardhi kwani kufanya hivyo wanaichonganisha serikali na wananchi badala ya kufanya maendeleo.

Immaculata Tenga, akipokea hati ya umiliki wa ardhi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, leo baada ya kusota kwa miaka kadhaa.

Ametoa kauli hiyo Julai 12,2024 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kabla ya kukabidhi hati kwa wananchi watatu ambao wamezisotea kwa muda mrefu kutokana na kuzungushwa na wataalamu wa idara hiyo.

“Uhusiano baina ya wananchi na serikali ni muhimu,mwananchi mmoja ameufuatlia stakabadhi ya hati kwa miezi sita hapo ardhi,wanatengeneza mazingira ya kufanya jambo liwe gumu ili kuwakatisha tamaa,wanatengeneza wapate rushwa,hawa wanatugombanisha na wananchi,”amesema Mtanda.

Amesema watumishi hao wa umma wasijigeuze mangimeza,wafanye kazi ya kuweka taswira nzuri ya CCM na serikali kwa wananchi kwa kutatua kero zao kwa wakati badala ya njoo kesho, njoo kesho.

“Tumsaidie Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, ana majukumu mengi.Wafanyeni kazi tuwatendee haki,haya mnayowafanyia mtafanyiwa pia,watendeeni wema nanyi mtalipwa kwa wema,”amesema Mtanda.

Anna Andrew ambaye pia ni mjane akieleza jinsi alivyohaingika kupata hati kwa miaka miwili kutoka Idara ya Ardhi Manispaa ya Ilemela, kabla ya kukabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda

Amesema viongozi wa serikali za mitaa baadhi badala ya kufanya maendeleo wanasababisha migogoro kwa kuuza viwanja na kutengeneza miliki pandikizi,hivyo wanaichonganisha serikali na wananchi,uchaguzi utakapofika wataachwa kwa sababu wanashusha mvuto wa CCM na serikali yake.

Mkuu huyo wa Mkoa pia ameagiza kuwe na rejista ya utatuzi wa migogoro ya ardhi jinsi ilivyotatuliwa kwa sababu CCM ikishindwa na serikali kuondoka madarakani sababu ya kero ya ardhi ama maji yeye atabaki wapi.

Pia wananchi wanayo haki ya kusikilizwa na hivyo Halmashauri na Mkuu wa Wilaya wakitoa huduma nzuri wataitendea haki serikali yao.

“Lazima nipambane na wewe unayeifitinisha serikali na wananchi,unataka kuweka kitumbua chetu mchanga na ikitokea serikali ikaondoka madarakani,sina hakika nani anayekuja.Pia wenyeviti wa mitaa wanauza viwanja na kusababisha migogoro,hawasomi mapato na matumizi bora waondolewe,”amesema Mtanda.

Wananchi waliokuwa wakizungushwa kupewa hati zao licha ya kufanya malipo wakiambatanisha na nyaraka muhimu, Immaculata Tenga na Anna Andrew (wajane) pamoja na Kimenye Gisimba wamemshukuru Mtanda kwa kutatua kero yao ndani ya siku moja.

“Tangu mwaka 2015 nafuatilia hati, kila nikija ardhi wananiambia njoo kesho njoo kesho,kwa kweli Rais Samia ameleta mkuu wa mkoa anayefahamu kutatua kero za wananchi, nilivyofuatilia hati kwa muda mrefu, Mungu akubariki uendelee kufanya kazi yako kama ulivyofanya kwetu,”amesema Tenga.

“Nimefuatilia hati halmashauri kutoka kwa miaka miwili nikisafiri kutoka Dar es Salaam, leo naona miujiza kuipata ndani ya siku moja.Nilitakiwa kulipa sh. 180,000 tu lakini sikupewa ushirikiano na baadhi ya watumishi wa ardhi,mbona ningelipa tu,”amesema Andrew.

Ameongeza kuwa kazi hiyo ni ya watu (umma) na wajane wanahangaika kupata haki zao, hivyo aliiomba serikali iwakumbuke na kwamba Mwanza imepata baba wananchi wanapaswa wajisifu.

“Nilivyomsikiliza Mkuu wa Mkoa natamani kurudi tena Mwanza,nilihama sababu ya kuchukizwa na kuumizwa na vitu vingi sasa natamani kurudi,ingekuwa ni kupiga kura ningepiga ili Mkuu wa Mkoa huyu (Said Mtanda) aendelee kubakia hapa,”amesema mjane huyo.

Naye Gisiba ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Ualimu Murutunguru, amesema licha ya kulipia gharama za hati na kuwasilisha nyaraka bado hakupewa kwa miezi sita, kila akifuatilia anaambiwa njoo kesho au nyaraka zimepotea,amepongeza Mtanda kwa kuwawezesha kupata hati zao ndani ya siku moja.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masala amesema wamepokea ushauri wa kuonesha watumishi waliopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi hasa viongozi wanaosiammia watumishi wa chini yao.

“Hapa ulikuwa ukizungumza na familia yako,wapo wengi wanapata usumbufu na nimepata fadhaa,mengi yanaletwa moja kwa moja idara ya ardhi hayafiki kwa Mkuu wa Wilaya,hivyo tutakumbushana majukumu kwa mujibu wa taratibu na tunakuahidi kukutekeleza maagizo yako,”amesema.