September 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiwanda cha Gloves Idofi kielelezo cha mageuzi makubwa uongozi wa Rais Samia

Na Reuben Kagaruki, Timesmajiraonline,Njombe

MTANZANIA yeyote akifika kwenye kiwanda cha kuzalisha mipira ya mikono (Gloves) kilichopo Idofi, Makambako, mkoani Njombe, kinachosimamiwa na Bohari ya Dawa (MSD) atakuwa shuhuda wa juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha bidhaa za afya zinazalishwa hapa nchini.

Kiwanda hicho ambacho kimeanza uzalishaji Februali, mwaka huu ni alama ya mageuzi makubwa yanayofanywa na Rais Samia ya kuhakikisha bidhaa za afya zinazalishwa nchini.

Juhudi hizo zinazofanywa na Serikali za Rais Samia pamoja na mambo mengine zinalenga kuhakikisha Serikali inaondokana na matumizi makubwa ya fedha za kigeni kuagiza bidhaa za afya nje ya nchi.

Kiwanda MSD Idofi kilianz Oktoba 4, 2020 katika kijiji cha Idofi, Makambako. Kiwanda hicho kimejengwa kwenye eneo lenye ukubwa hekari 38 ambalo ni mali ya MSD.

Kiwanda hicho ni mojawapo ya viwanda vitatu vilivyopo MSD ambavyo vinaendelea na uzalishaji. Kiwanda cha kwanza kilikuwa ni cha kutengeneza barako, ambacho kipo Keko, jijini Dar es Salaam.

Kiwanda cha pili kuanzishwa na MSD ni cha kutengeneza barakoa aina ya M 95, viwanda hivyo viwili vilifuatiwa na kiwanda cha MSD Idofi, ambacho kiliwekwa jiwe na msingi Oktoba 2023 na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango.

Baada ya kuwekwa jiwe la msingi kilikamilisha hatua hatua zote, ambazo zilikuwa zinahitajika kukamilishwa katika maeneo ya uhifadhi na maabara.

Kiwanda cha gloves Idofi

Baada ya kukamilika hatua hizo Februali, mwaka huu kilianza rasmi uzalishaji na kina uwezo wa kuzalisha gloves kwa saa 24 kwa siku tatu mfululizo na baada ya hapo kifanyiwa Service kwa saa 24, halafu kinaendelea kufanyakazi kwa saa 24.

Kiwanda hicho kinazalisha viwanda gloves za kutamaniwa na kukubaliwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Kuanzishwa kwa kiwanda hicho mafanikio makubwa yanayotokana maboresho yanayofanywa na MSD kiutendaji ambayo yamewezesha gloves ambazo zilikuwa zikiagizwa nje ya nchi kuanza kuzalishwa chini.

Mageuzi hayo yanayothibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, yameshuhudiwa na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini waliokuwa kwenye ziara ya kutembelea na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na MSD katika Kanda ya Iringa na Kanda ya Dodoma, wiki iliyopita.

Wakati wa ziara hiyo wahariri hao wa vyombo vya habari walijionea uzalishaji gloves kupitia hatua zote 15 za uzalishaji bidhaa hizo.

Kuanza uzalishaji katika kiwanda hicho ni matokeo ya kuanzishwa kwa Kampuni Tanzu ya MSD Medipham Manufacturing CO LTD, ambayo ndiyo mmiliki wa viwanda hivyo vitatu, ambavyo vingine vya kuzalisha dawa na pamba vikiwa mbioni.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kiwandani hapo, Kaimu Meneja wa kiwanda hicho, Shiwa Mushi anasema uwezo wa kiwanda ni kuzalisha jozi 10,000 za gloves kwa saa moja sawa na jozi milioni 86.4 kwa mwaka.

Anafafanua kwamba uzalishaji wa gloves za kuuza ulianza rasmi baada ya MSD kupata cheti cha Ithibati ya Ubora pamoja na cheti cha usajili wa bidhaa za kuu kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Kwa mujibu wa Mushi kiwanda hicho kinazalisha gloves kwa kutumia malighafi ya utomvu inauotokana na mmea wa mpira.

Mushi anasema ili gloves ziweze kuzalishwa na kuwa na ubora unaotakiwa zinapitia hatua 15.

Hatua ya kwanza, anasema ni kuoshwa kwa mikono ili kuondoa vimelea, hatua ya pili ni mikono hiyo kukaushwa kwenye mashine maalum na hatua ya tatu ni mikono kuingia katika kemikali maalum ambayo ni kwa ajili ya kuandaa mkono uweze kupokea utomvu.

Mushi anataja hatua ya nne kwamba ni kukausha tena mikono na hatua ya tano ni mikono kupitishwa katika kemikali ya utomvu na hatua ya sita ni mikono kukaushwa tena.

Anataja hatua ya saba ni mikono kuingia katika kemikali maalum ambayo inafanyakazi ya kuondoa vimelea na hatua ya nane ni kuhakikisha ni mikono iliyochanganyikana na utomvu kuingizwa kwenye eneo maalum ili kama kuna kemikali zozote ziweze kuondolewa, kuimarisha ubora wa gloves na kuondoa vimelea na hatua ya tisa kuingizwa kwenye mfumo maalum kwa ajili ya kuandaa pindo za gloves.

Hatua ya 10 ni kukaushwa na hatua ya kumi na moja ni gloves kuingizwa maabara kwa ajili ya kuangalia ubora wake na hatua 12 inaingizwa katika hatua ya ukaushwaji.

Hatua ya 13 ni gloves kupelekwa katika chumba maalum kwa ajili ya uhakiki wa bidhaa, hatua ya 14 ni kuziweka katika vifungashio na hatua 15 ni kupelekwa gloves kwenye maghala kwa ajili ya kusubiri kusambazwa kwa mujibu wa taratibu za MSD

Afisa Uhusiano Mkuu wa MSD, Etty Kusiluka, Anasema gloves hizo zinazalishwa na wazawa (Watanzania).

Aidha, anafafanua kwamba awali MSD ilikuwa na majukumu matatu, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya kwa ajili vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na baadhi vya binafsi ambavyo vimeidhinishwa na Wizara ya Afya.

Hata hivyo, anasema hivi karibuni Sheria ya MSD ilifanyiwa mabadiliko na kuongezewa jukumu la nne la kuzalisha, hivyo hivi sasa MSD inazalisha, inanunua, inatunza na kusambaza bidhaa za afya kwa hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma na zile zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.

“Lakini pia tunatoka nje ya mipaka tukipata wateja kama mnavyojua tunahudumia zile nchi zilizopo kwenye ukanda wa SADC,” anasema Kusiluka.

Anasema baada ya hilo, MSD iliona ni vyema ikaunda kampuni tanzu ambayo itakuwa na jukumu kubwa la kusimamia viwanda vyote ambavyo vipo chini ya MSD.

Kwa mujibu wa Kusilulika hivi karibuni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amezindua Kampuni Tanzu ambayo itakuwa inashughulikia viwanda vyote vya MSD.

Aidha, anasema alizindua Bodi ambayo itasimamia shughuli zote za uendeshwaji wa viwanda vya MSD.

Anasema viwanda hivyo vitatu tayari vimeanza kazi. Viwanda ambavyo vinafanyakazi ni kiwanda cha Barakoa kilichopo Keko, kiwanda cha kiwanda cha kuzalisha barakoa za M 95 na kiwancha cha gloves Idofi.

Aidha, anasema vipo viwanda ambavyo vipo mbioni kuanzishwa, ambavyo ni pamoja ni viwanda vya dawa vitakavyokuwa Zegereni, mkoani Pwani na viwanda vingine vitakavyokuwa vinazalisha malighafi ya pamba vitakuwa mkoani Simiyu.

Mwonekano wa kiwanda

“Hii yote ni katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuwa na viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya nchini kwa zile ambazo zinawezekanika na malighafi zake zikapatikana kwa urahisi,” anasema Kusiluka na kuongeza;

“Hii itasaidia pia Serikali kuondokana na matumizi makubwa ya fedha za kigeni ambazo zimekuwa zikitumika kuagiza vifaa za afya kutoka nje ya nchi.

Kama mnavyofahamu zaidi ya asilimia 85 ya bidhaa za afya ambazo MSD inahudumia wateja wake zinatokana nje ya nchi.

Kwa hiyo hii itakuwa hatua moja wapo ya kuiwezesha Serikali kuanza kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuhakikisha bidhaa za zinapatikana kwa uhakika, tutakuwa na uhakika kwamba zipo na zinapatikana kwa wakati kwenye kwa wateja wetu.”

Kwa mujibu wa Kusiluka hiyo itasaidia kama ikitokea mlipuko kama ilivyokuwa wakati wa Covid 19, ambapo anga zilifungwa.

“Ikitokea janga kama hilo hatutakuwa na sababu ya kuangaika tena, viwanda kama hivi vinapoanzishwa Serikali inakuwa imeweka lengo la kuwezesha nchi kujitegemea katika baadhi ya bidhaa za afya na kadri tutakavyokuwa tunaendelea tutazidi kuwekeza zaidi, kwani Serikali ipo tayari kuhusisha wabia wengine ambao wako tayari kuwekeza katika masuala mazima ya uzalishaji bidhaa za afya kwa kushirikiana na MSD,” anasema Kusiluka.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, anasema hadi kufikia Juni 2024, Kiwanda kimeweza kuzalisha jumla ya gloves zaidi ya milioni 4.

Aidha, anasema kiwanda hicho kimetoa ajira 136 kwa wakazi wa eneo la Makambako na kufanya ununuzi kwenye kampuni mbalimbali ziliozopo eneo la Makambako.

Kwa kutengeneza mipira ya mikono ya kiuchunguzi “examination gloves” pekee kiwanda kitaweza kuokoa zaidi ya sh. bilioni 11.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wahariri walipongeza uamuzi wa MSD kuanzisha kiwanda hicho hatua ambayo sasa inafanya MSD kuachana na kuagiza Gloves kutoka nje ya nchi.

“Haya ni mageuzi makubwa ndani ya nchi yetu,ukifika pale Idofi ndipo utajua MSD inafanya mambpo makubwa katika nchi yetu kwa ajili ya kulinda afya za Watanzania,” alisema Mhariri wa Jamhuri, Stella Aroan.

***Bohari ya Dawa (MSD)

Bohari ya Dawa (MSD) ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Sheria ya Bohari ya Dawa Na.13 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2021 ikiwa na majukumu manne.

Majukumu hayo ni Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za umma na binafsi zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.

Bohari ya Dawa inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya 8,224 kutoka vituo 7,662 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la vituo 562 nchi nzima kupitia Kanda zake 10 zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.