September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka mitatu ya Rais Samia chachu mafanikio ya Halmashauri Igunga

Na Lubango Mleka.Timesmajiraonline

MARA ya kwanza kuhutubia Taifa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliwaondoa wasiwasi Watanzania kwamba japo kuwa yeye ni wa jinsi ya kike, ndiye Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wasiwe na mashaka naye katika kuendeleza gurudumu la Urais nchini.

Alitambulisha salamu mpya nchini iliyobeba kauli mbiu yake akasema, nikisema “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, mtaitikia “Kazi Iendelee”.

Ni kweli kabisa katika miaka mitatu ya uongozi wake tunaiona kazi ikiendelea na hajaacha kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ili kufungua uchumi wa Tanzania, ikiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa reli ya mwendo kasi, ujenzi wa madaraja kama vile Tanzanite na Wami, ujenzi wa Barabara za lami na Bandari kavu.

Kwa upande wa Serikali za Mitaa miradi ya Afya, Elimu, Maji, Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Madini na Uchumi Rais Dkt.Samia amekuwa akielekeza pesa nyingi katika kuimarisha huduma muhimu ambazo Serikali imeazimia kuhakikisha zinawafikia wananchi kwa ubora na ufanisi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Selwa Abdalla Hamid anasema kuwa, Igunga inayo mambo mengi ya kujivunia ndani ya miaka mitatu ya utawala wa Rais Dkt. Samia katika ufikishaji wa huduma za Afya, Elimu, Kilimo, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na Utawala kwa Jamii.

“Kwa niaba ya Wanaigunga nipende kutoa shukrani zangu za pekee kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Halmashauri ya Wilaya ya Igunga imepokea jumla ya sh. 26,417,666,725.24 ambazo zimeweza kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo, ” anasema Hamid.

Kupitia fedha hizo za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Halmashauri ya Wilaya Igunga imeweza kupata mafanikio mengi kupitia sekta mbalimbali.

SEKTA YA ELIMU YA AWALIMU NA MSINGI

Kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ilikuwa na jumla ya shule za msingi za Serikali 138 lakini kwa sasa ina jumla ya shule 148 za msingi, ongezeko hili ni kutokana na fedha ambazo Serikali ya Dkt. Samia imeweze kuipatia Halmashuri hii.

“Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 tumeweza kujenga shule mpya mbili za msingi ambazo zipo katika kiwango bora na wanafunzi wameanza kusoma katika shule hizo, pia tumeweza kuwahamisha wanafunzi kutoka kwenye shule zilizokuwa na mrundikano na kuwapunguzia umbali, ” alisema Mkurugenzi Hamid.

Kwa upande wa vyumba vya madarasa kabla ya Rais Dkt. Samia vilikuwa 980 na kwa sasa kuna vyumba 1,083, ambapo jumla ya walimu 1,283 walikuwepo hapo awali na kwa sasa kuna jumla ya walimu 1,324 katika shule za msingi, huku uwajibikaji wa walimu hawa umechangia kwa kiwango kikubwa ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba kutoka asilimia 64.28 na kufikia asilimia 77.74.

ELIMU SEKONDARI

Kwa kipindi cha awamu hii ya sita, idadi ya shule za sekondari za Serikali imeomgezeka kutoka shule 30 hadi shule 39 sawa na ongezeko la asilimia 30, mwaka 2021 kulikuwa na jumla ya wanafunzi 11,052 na imeongezeka na kufikia 13,794 kwa mwaka 2024 sawa na asilimia 24.

Idadi ya vyumba vya madarasa kwa elimu ya sekondari imeongezeka kutoka 335 na kufikia vyumba 498 ambayo ni ongezeko la vyumba 133, kulikuwepo na walimu 362 hapo awali kwa sasa kuna jumla ya walimu 495, uwajibikaji wao umechangia kwa kiasi kikubwa cha ufaulu kwa kidato cha pili kutoka asilimia 80 hadi asilimia 91, kidato cha nne ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 95 hadi asilimia 99 na kwa kidato cha sita umeendelea kuwa asilimia 100 katika kipindi chote cha Serikali ya awamu ya sita.

Ari ya Walimu kufanya kazi kwa juhudi imetokana na Serikali ya Awamu ya Sita kuwalipa stahiki zao, ikiwemo likizo, kupanda madaraja na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Kwa upande wa hosteli za wanafunzi idadi ya shule za Serikali zilizokuwa zinatoa huduma ya hosteli kwa wanafunzi imeongezeka kutoka shule 10 hadi kufikia shule 17, jambo ambalo limewasaidia wanafunzi waliokuwa wanatoka maeneo ya mbali, imepunguza utoro na kuongeza ufaulu.

SEKTA YA AFYA

Hali ya miundombinu ya afya na upatikanaji wa huduma za afya kabla ya awamu ya sita, vilikuwepo vituo vya afya vinne (4) kwa sasa vimeongezeka na kufikia vituo vya afya sita (6), kulikuwepo na Zahanati 53 na zimeongezeka na kufikia 64 hii ni kutokana na jitihada kubwa za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma za afya karibu.

“Kabla ya awamu ya sita Hospitali yetu ya Wilaya ya Igunga haikuwa na jengo la watu mahututi (ICU) lakini chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupatia fedha kiasi cha sh. 383,022,684.00 kwa ajili ya kujenga jengo la wagonjwa mahututi ambalo kwa sasa limekamilika na huduma zinatolewa,”

“Aidha kwa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita jumla ya sh. 3,170,819,130.00 zimetumika kwa ajili ya kununua dawa katika Bohari ya dawa (MSD) ambayo ni ruzuku (Receipt in kind), na hali ya upatikanaji wa dawa imeongezeka kutoka asilimia 80 hadi asilimia 90, pia tunaendelea na ujenzi wa majengo manne (4) ambayo ni jengo la OPD, wodi ya Wanaume, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la mionzi kwa gharama ya sh. 900,000,000, alisema Hamid.

Huduma ya mama wajawazito na Watoto imeimarika na idadi ya vifo vya akina Mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi imepungua kutoka 92 kati ya Wamama 100,000 mwaka 2020 hadi 57 kati ya Wamama 100,000 kwa mwaka 2023, idadi ya vifo vya Watoto wachanga vimepungua kutoka 15 kwa Watoto 1000 mwaka 2020 hadi vifo vinne (4) kati ya Watoto 1000 kwa mwaka 2023.

Hamid alimaliza kwa kusema kuwa, vifo vya Watoto chini ya miaka mitano imepungu kutoka vifo 13 kati ya Watoto 1000 mwaka 2020 hadi kufikia Watoto sita (6) kati ya Watoto 1000 mwaka 2023, mafanikio haya yote yamechangiwa na uboreshaji mkubwa wa huduma za afya ambayo imefanywa na Serikali ya awamu ya sita.