November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

The Desk & Chair Foundation yawapunguzia mzigo wanafunzi 150 wa kidato cha tano

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

TAASISI ya The Desk & Chair Foundation imetoa msaada wa vifaa vya elimu vyenye thamani ya milioni 30 kwa wanafunzi 150 waliochaguliwa kujiunga na masomo ya elimu ya sekondari kidato cha tano mwaka huu .


Akizungumza leo Julai 6,2024 baada ya kukabidhi vifaa hivyo vya elimu, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Dkt. Alhji Sibtain Meghjee amesema msaada huo utapunguza gharama za mahitaji ya shule kwa wanafunzi hao wanaojiunga na masomo ya kidato cha tano.

“Mahitaji yote ni milioni sh.30 ambapo vifaa tulivyokwisha kabidhi hadi sasa ni madaftari,mabegi mashuka,vyandarua na rim kwa wanafunzi 120 kati ya 150 ambao ni nusu ya 300 walioomba,”amesema.

Dk.Alhaji Sibtain amesema wastani wa mahitaji kwa kila mtoto ni sh. 650,000 lakini wamewapatia vifaa vya thamani ya sh.200,000 ili kuwapunguzia mzigo wa gharama za kununua mahitaji hasa wa familia zisizo na uwezo.

“Changamoto maombi ni mengi kuzidi bajeti iliyotolewa na wafadhili, rai yangu serikali ione namna ya kupunguza baadhi ya vifaa ili kuwapunguzia mzigo wazazi ili kuwapa fursa watoto wanaochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano kumudu gharama za mahitaji,”amesema.

Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa msaada huo wa vifaa,Lucia Joseph ameishukuru taasisi hiyo kwa kuwasaidia vifaa mbalimbali vya elimu huku akiahidi kufanya vizuri katika masomo na mitihani yake ya mwisho.

“Binafsi familia yangu haina uwezo kutokana na kipato duni kiasi kwamba sikuwa na uhakika wa kwenda shule licha ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano, vifaa ni vingi ambavyo hesabu yake ni zaidi ya sh.600,000.Naishukuru taasisi hii kwa kubeba sehemu ya jukumu la wazazi,”amesema.

Mwanafunzi huyo ameiomba serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuangalia upya mahitaji ya shule kwa wanafunzi wa kidato cha tano kwa sababu ya gharama ya vifaa iko juu kiasi kwamba watoto wa familia duni ni vigumu kuendelea na masomo.

Aidha baadhi ya wazazi wamesema shule nyingi zimeagiza kila mtoto kwenda rimu mbili za karatasi za A4,jembe,panga,kwaja (fyekeo) dawa na brusha za chooni, fagio na kuhoji vifaa hivyo vinapelekwa na watoto kila mwaka vinapelekwa wapi?

“Hapa serikali inapaswa kufanya uchuguzi na ukaguzi wa vifaa wanavyotakiwa wanafunzi kwenda navyo siku ya kuripoti shuleni vipo ama ni biashara ya wakuu wa shule maana haiwezekani kila mwaka mtoto anakwenda na jembe,rimu,panga, fyeo na reki ,”amesema Moses Masau.

Mzazi mwingine James Masambu amesema uchunguzi alioufanya alibaini rimu za karatasi za A4 zina soko,zinazotumika ni chache nyingi zinarudi kuuzwa mitaani kadhalika majembe, mapanga,mafyekeo na dawa za chooni,ni biashara inafanywa na wakuu wa shule mtoto asipokwenda navyo hapokelewi.

“Serikali inatoa elimu bure lakini walimu wanaifanya elimu hiyo ionekane inagharamiwa na vifaa kwa manufaa yao.Tunamwomba Waziri mwenye dhamana alitolee tamko vinginevyo wananchi wataona elimu bure ni ulaghai wa siasa,”amesema.