September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sukari yamuibua Mgeja, atoa ushauri kwa Rais Dkt. Samia

*Awaonya wanasiasa wanaotumia suala hilo kujipatia umaafuru kisiasa, asema malumbano ya sukari hayajaanza leo, apongeza utendaji wa Waziri Bashe

Na Suleiman Abeid,Timesmajiraonline Shinyanga

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameombwa kuangalia uwezekano wa kulifanya zao la miwa inayozalisha sukari kuwa zao la kimkakati ili kuondoa changamoto ya uhaba wa sukari unaojitokeza mara kwa mara nchini.

Ombi hilo limetolewa jana kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chama hicho mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja, wakati wa mahojiano yake maalumu na waandishi wa habari mjini Kahama.

Mgeja amesema mbali ya zao hilo kuwa la kimkakati lakini pia Serikali inapaswa kuanza kuwahamasisha Watanzania ili wawekeze kwenye sekta ya viwanda vikubwa vya sukari, vya kati na vidogo vidogo ili sukari iweze kuzalishwa kwa wingi hapa nchini kwa vile mali ghafi (miwa) itakuwepo ya kutosha.

“Binafsi mimi sifurahishwi na haya malumbano yanayoendelea hivi sasa hapa nchini kwetu, ambayo yamesababishwa na changamoto ya uhaba wa sukari kuadimika kipindi fulani, kiasi cha baadhi ya wanasiasa kuibeba agenda hii na kuifanya mtaji wa kisiasa,”

Tiba ya changamoto hii ni kumuomba Rais Samia sasa atangaze kwamba kilimo cha miwa inayotengeneza sukari kipewe kipaumbele, watu walime miwa mingi, na zao hili liwe la kimkakati, naamini baada ya kipindi kifupi uhaba wa sukari hapa nchini utabaki kuwa historia, na tutaweza kuuza hata nje ya nchi,” ameeleza Mgeja.

Hata hivyo Mgeja ameendelea kueleza kuwa changamoto mbalimbali zinazojitokeza hapa nchini zinapaswa kupatiwa utatuzi kwa Watanzania wenyewe kushauriana na kupendekeza njia sahihi za kuzimaliza badala ya kuzigeuza mtaji wa kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa kuwachafua wenzao walioko madarakani.

“Haya malumbano ya uhaba wa sukari hayajaanza leo, hata kipindi cha Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa yalijitokeza, sasa tatizo hili limekuwa likijirudia rudia nafikiri utatuzi wake ni kuzalisha sukari ya kutosha hapa nchini, na wanasiasa waache kulifanya mtaji wa kisiasa,”

“Tumesikia wenyewe hivi karibuni sakata ambalo limetokea kule bungeni, ndugu yetu Luhaga Mpina ameibua hoja ya kumlaumu waziri Bashe akimtuhumu kulidanganya bunge kuhusiana na suala la vibali vya sukari, mbali ya kutoa hoja hiyo bungeni lakini alitoka nje na kuongea na vyombo vya habari, ikaleta shida,” ameeleza Mgeja.

Amesema yapo mambo ambayo yamewahi kufanyika hapa nchini bila kufuata utaratibu wa kisheria lakini kwa nia njema ya kukabiliana na changamoto iliyojitokeza kwa wakati huo lengo ikiwa ni kuwasaidia watanzania na watu walikaa kimya hawakulaumu wala kumshutumu kiongozi ye yote.

Mgeja amefafanunua kuwa alichopaswa kufanya Mpina ilikuwa ni kukaa na Serikali na kuonesha mapungufu ambayo yeye anaamini ni mapungufu na kushauri nini kifanyike badala ya kulalamika na kumlaumu waziri mwenye dhamana na wizara ya kilimo kwamba amefanya makosa.

“Nimuombe kijana wangu ambaye kwa kweli nimemkuza mimi mwenyewe kisiasa, Mheshimiwa Mpina, namuheshimu sana, lakini hanifurahishi hata kidogo kuona kila saa anafukua makaburi badala ya kukaa chini na kusaidiana na Serikali kwa ujumla kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi, ili tutoke hapo na kusonga mbele,”

“Mpina anapaswa atambue kwamba katika kuongoza nchi iko busara inahitajika zaidi, si kila jambo linalotokea ndani ya Serikali lazima lisemwe hadharani, Serikali haiko hivyo, mbona kipindi chao akiwa Waziri walichoma mamilioni ya vifaranga vya kuku vilivyotokea Kenya, Je hiyo ilikuwa busara? Ni bora vingerudishwa vilikotoka,” ameeleza.

Katika hatua nyingine, Mgeja alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchapa kazi na wasipoteze muda kushabika mambo ambayo hayana tija kwa Taifa ambayo huwa na mlengo wa kisiasa zaidi, na kwamba anavyoelewa yeye kwenye sakata hili la sukari hakuna fedha taslimu ambazo zimeibwa ndani ya Serikali.

Amesema wizara hizi haziongozwi na malaika, hivyo yapo makosa madogo madogo ya kiutendaji ambayo yanaweza kujitokeza na hata huko nyuma watanzania waliona yapo mambo yalifanyika bila kufuata utaratibu lakini watu walikaa kimya na hata ripoti ya upotevu wa sh. bilioni 1.5 watu hawakuvalia njuga kama hili la sukari

“Tatizo letu ni viongozi wetu kutokupenda kushirikiana na kuwa kitu kimoja, shida yetu ni umasikini wa mawazo, wavivu wa kufikiri lakini pia nafsi zetu zina roho mbaya, roho za chuki, hatuna upendo miongoni mwetu, tuna siasa za kuviziana, hili linaturudisha nyuma kama Taifa,”

“Ushauri wangu tuvipige vita vitendo hivi ambavyo vinaturudisha nyuma kama Taifa, tulete mapinduzi ya fikra, tukileta mapinduzi ya fikra Tanzania kwenye neema itasonga mbele, maendeleo na maisha bora kwa kila Mtanzania itawezekana,” alieleza Mgeja.

Ameendelea kueleza kuwa moja ya wizara ambazo huko nyuma zilikuwa zikiyumba ni wizara ya kilimo ambayo tangu alipokabidhiwa, Waziri Hussein Bashe kidogo wizara hiyo imeanza kuonesha mafanikio makubwa ikiwemo kuweka mipango mikakati ya kuwasaidia wakulima husasan vijana wa kitanzania.

“Kuanzia Serikali ya awamu ya tatu malumbano yalikuwepo hasa kwenye wizara hii ya kilimo upande wa sakata la uhaba wa sukari, hivyo binafsi nashauri tukiwa na uzalishaji mkubwa wa sukari haya malumbano ya kila mara hayatatokea tena,” amesema

“Malumbano haya mara nyingi yamekuwa yakitumiwa na wanasiasa kama mtaji wa kisiasa, na wengine kutaka kutoana kafara kwa watendaji na viongozi walioko ndani ya wizara, sasa hili lifike wakati liishe, na tutafanikiwa tu kwa kuongeza uzalishaji wa kutosha wa sukari hapa nchini, nakumaliza changamoto za kila mara,” amesema.