September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GST yaleta tabasamu kwa wachimbaji Madini ya Tanzanite Mirerani

Na Mary Margwe, Timesmajira Online,Simanjiro

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inayotumia ndege nyuki kufanya utafiti wa kubaini maeneo yenye madini ya Tanzanite Mji Mdogo wa Mirerani umemsaidia mchimbaji moja kwa moja kuweka mtaji wake mahali ambapo anategemea kukutana na kitu anachokitafuta badala ya kufanya kazi kwa kubahatisha kama ilivyokua awali.

Hayo yamebainishwa Jana Juni 23,2024 na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Franone Mining Ltd, Vitus Ndakize wakati wakipatiwa majibu ya awali ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo katika Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, ambapo tayari eneo la Kitalu C na D kimefanyiwa utafiti huo.

Ndakize amesema utafiti utakuwa chachu kwa wachimbaji wa Madini ya Tanzanite, kwani utapunguza gharama kwa kuchimba huku wakifuta taarifa zilizopatikana kupitia GST na kuepuka uchimbaji wa kubahatisha.

Mchimbaji Mdogo wa Madini ya Tanzanite wa kitalu D, Paulo Mwanache amesema siku zote walikua wakichimba madini kwa kubahatisha baada ya kufanyika kwa utafiti huo wamepata mwelekeo wa kuona miamba iliyolala na jinsi watu wanaweza kupata madini kiurahisi.

“Utafiti umetuonesha maeneo yenye miamba iliyolala na wapi penye madini mengi na wakatueleza sababu ya madini kuungua chini kabla ya uzalishaji wake hivyo utafiti huo umekuwa ni njia rahisi kwetu kufanya uchimbaji usiokua na hasara tofauti na awali,” amesema Mwanache.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa GST, Dkt. Mussa Budeba,amesema utafiti huo utasaidia urahisi wa upatikanaji wa madini ya Tanzanite katika maeneo husika.

Dkt. Budeba amesema utafiti huo utawaepusha wachimbaji wadogo na wa kati juu ya hasara ya kuchimba kwa mazoea, maeneo yasiyo na madini kwani kwa awamu ya kwanza wamepima kwenye eneo la Kitalu C na D.

Aidha Dkt. Budeba amesema wanatarajia kufanya utafiti kwa asilimia 50 kwenye maeneo yote nchini hadi ifikapo mwaka 2030 ambapo kwa sasa Utafiti umefanywa kwa asilimia 16 kwa baadhi ya maachimbo.

“Waziri wa Madini Anthony Mavunde amekuja na maono ‘vision’ ya 2030 madini ni maisha na utajiri, kwa kufanya utafiti pia tumeongezewa bajeti,” amesema Dkt. Budeba.

Ofisa madini Mkazi wa Mirerani, Nchagwa Marwa amesema utafiti huo wa awali uliofanywa na GST, umehusisha vitalu viwili vya C na D na utafiti ujao utahusisha maeneo mengine yaliyobaki.

Marwa amesema GST watarejea tena kwa kuongeza wigo wa kufanya utafiti kwenye maeneo yote ya machimbo ya madini ya Tanzanite Mji Mdogo wa Mirerani.