September 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makongoro ataka fedha zinazokusanywa zifikishwe benki

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kalambo Shafi Mpenda kuhakikisha fedha zote zinazo kusanywa zinawasilishwa benki kwa wakati huku watumishi waliotumia fedha mbichi kuchukuliwa hatua.

Huku akiipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati inayoridhisha kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

Makongoro ameyasema hayo kupitia kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Kalambo kuhusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hyesabu za Serikali kwa mwaka 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

Ambapo amepiga marufuku Halmashauri kutumia fedha mbichi na kuagiza hatua dhidi ya watumishi waliotumia fedha hizo na kufanya udanganyifu kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

Amesema kuwa ufuatiliaji uliofanywa na Mkoa umebaini kuwa yapo mapato katika mfumo wa LGRCIS yaliyokusanywa na Watendaji wa Halmashauri katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023 kiasi cha zaidi ya milioni 243.4 ambayo haijawasilishwa benki hadi sasa.

“Nikuagize Mkurugenzi kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa na wahusika wanachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa kuzingatia kanuni ya 36-37 ya kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022,’’ Makongoro.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Wambura Sundy, amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 halmashauri imefanikiwa kukusanya fedha kiasi cha zaidi ya bilioni 1.68 sawa na asilimia 83 huku kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ikifanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 1.71 sawa na asilimia 71 ya bilioni 2.412 kiasi ambacho kilikasimiwa kukusanywa kwa mwaka wa fedha 2023/2024.