November 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yashauriwa kufanya mazoezi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

JAMII imeshauriwa kuwa na utaratibu malumu wa kufanya mazoezi mara kwa mara kwa lengo kuweka mwili sawa ili kujikinga na maradhi yasioambukiza.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Azzan Sports Foundation, Iddi Azzan wakati wa tamasha la michezo liliofanyika uwanja wa Barafu uliopo Magomeni Makuti, jijini Dar-es-Salaam.

‘’Bonanza hili malumu la kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi, tumeandaa sisi Barafu Jogging kwa kushirikiana na Chama cha Jogging Kinondoni(KIJA) pamoja na Wizara ya Afya,”amesema Azzan.

Aidha, Mbunge huyo wa zamani wa Kinondoni, ameishauri jamii kufanya mazoezi kwa ajili ya kujikinga na maradhi yasioambukiza kwa kuwa mazoezi ni muhimu na yanasaidia kuimarisha afya kuanzia kwa watoto mpaka watu wazima.

‘’Mazoezi ni muhimu, tunapata ‘sapoti’ kufungwa mkono na serikali kupitia Wizara ya Afya,kauli mbiu yetu ya ‘Mtu Ni Afya’, lazima tuendelee nayo kwa kuwa bila afya huwezi kufanya chochote,”amesema.

Naye Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema lengo la Wizara ya Afya ni kuhamasisha ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya ‘Mtu Ni Afya’ iliozinduliwa na makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango na kusimamiwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Amesema wanaendelea kufanya uhamasishaji kwani mazoezi pekee yake hayatoshi lazima yaendane na ulaji chakula ulio sahihi.

‘’Tumekuwa tukifanya uhamasishaji wa kampeni ya ‘Mtu Ni Afya’ imejikita katika maeneo makuu matatu ambapo moja ni kupambana na magonjwa yasiokuwa ya kuambukiza kama kisukari, shinikizo la damu pamoja na saratani,’’ amesema.