October 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shule mbili za sekondari kujengwa Nyamrandirira na Bukumi

Fresha Kinasa, TimesMajira, Online, Musoma.

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa, Serikali imetoa fedha kiasi cha zaidi ya bilioni 1.1 kwa Kata mbili ambazo ni Nyamrandirira na Bukumi zilizopo jimboni humo kwa ajili ya kujengwa shule mpya za sekondari za Kata hizo.

Kila Kata imetengewa zaidi ya milioni 584.2 na kwa Kata ya Nyamrandirira shule hiyo itajengwa Kijiji cha Kasoma huku Kata ya Bukima itajengwa Kijiji cha Butata.

Hayo yamebainishwa Juni 20,2024 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge huyo kwa mujibu wa taarifa hiyo ametoa ushauri kwa viongozi wa serikali na chama wa Kata, Vijiji na Vitongoji wahamasishe wananchi wachangie nguvukazi ili miundombinu mingi ya elimu ipatikane kutoka kwenye fedha hizo.

Ambapo ameshauri pia maeneo ya ujenzi yasiwe na migogoro ya aina yoyote ile, na Wananchi wafuatilie matumizi ya fedha za ujenzi kwa ukaribu sana na ukamilike mapema ili ifikapo Januari mwaka 2025 sekondari hizo mpya zifunguliwe.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Prof. Muhongo amepokea maombi kutoka vijiji vitatu ya kujenga sekondari mpya
Ikiwemo Kijiji cha Kataryo, Kata ya Tegeruka, Kijiji cha Kiriba, Kata ya Kiriba
na Kijiji cha Mmahare, Kata ya Etaro.

Ambapo maombi hayo ameyakubali na baada ya Bunge ataenda kufanya harambee za kuanza ujenzi wa sekondari hizo.

Huku shule za sekondari zinazojengwa sasa hivi kwa nguvu za wananchi na viongozi wao ni Rukuba (Kisiwa), Kata ya Etaro, Nyasaungu, Kata ya Ifulifu,
Kurwaki, Kata ya Mugango na
Muhoji, Kata ya Bugwema ambapo serikali imeanza kuchangia kwa kutoa kutoa milioni 75.

Shule za sekondari 28 kati ya hizo za serikali ni 26 na binafsi 2 ndizo zinazotoa elimu kwa sasa, ndani ya Jimbo hilo lenye Kata 21 na vijiji 68.

“Lengo Kuu, Kila Kata iwe na sekondari mbili au zaidi, mfano Kata ya Nyamrandirira yenye vijiji vitano ifikapo Januari 2025 itakuwa na sekondari tatu kwenye vijiji vya Kaboni, Seka na Kasoma,”imeeza taarifa hiyo.

Nao Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini wameishukuru serikali kuendelea kuwapatia fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo za ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari,uboreshaji wa miundombinu ya elimu kwenye shule mbalimbali jimboni humo.