Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA),Mkoa wa Mwanza,limeishauri serikali kuhakikisha inalinda afya za binadamu kwa kuwaepusha na maradhi yanayoweza kusababishwa na kula nyama isiyofaa.
Pia limewakumbusha waislamu kuchinja kama ilivyo sheria ya dini na kuendelea kumcha Mwenyezi Mungu.
Ushauri huo umetolewa Juni 16, mwaka huu na Sheikh Alhaji Hasani Kebeke, amesema waislamu waache tamaa kwani baadhi yao wanachinja bila kujali afya za wanyama kama wana maradhi,hivyo wafuate sheria za nchi na dini wanapochinja mifugo kwani dhambi ya uhalifu ni dhambi tu hata wakijificha katika dini.
Sheikhe Kabeke amesema mifugo inayostahili kuchinjwa kwa watu wenye uwezo ni wanyama kama ngamia wakiwemo ng’ombe,mbuzi na kondoo ambao hawatakiwi kuwa waliokondeana,wagonjwa,dhaifu na waliokatwa masikio.
“Sheria inatutaka kuchinja ngamia,ng’ombe,mbuzi ama kondoo wawili weupe,hivyo nitoe wito kwa serikali kusimamia afya za binadamu,wakati wa kuchinja wananunuliwa ng’ombe wagonjwa watu watapata maradhi endapo sheria hazitasimamiwa kwa kigezo cha dini,”ameonya.
Kiongozi huyo wa kiroho amesema zipo taasisi ambazo watu wanaotaka kuchinja wanapaswa kujisajili ili ifahamike waumini wa dini hiyo na wengineo wanakula nyama yenye afya isiyo na magonjwa.
Wakati huo huo Sheikh Kabeke amesema Baraza la Eid Al Adhaa linafanyika leo Jumanne kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Amesema baraza hilo litafanyika majira ya saa tisa alasiri na kuwaomba wote watakaojaaliwa kuhudhuria.
More Stories
Watakiwa kupiga kura na kuondoka vituoni
Dkt.Mpango:Viongozi mtakaochaguliwa, uchaguzi wa serikali za mitaa tumieni nafasi zenu vizuri
Wananchi Nyamanoro Mashariki,Mkudi wajitokeza kupiga kura