October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kumpatia viungo bandia bodaboda aliyetekwa

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Serikali imesema itampatia Viungo Bandia kijana Lucas Mhambo mwenye umri wa miaka 24 mkazi wa Dumila Wilaya kilosa ambaye amepata ulemavu wa kudumu baada ya kutekwa na watu wanaodaiwa kuwa vibaka na alipofikishwa hospitali ililazimika kukatwa miguu na mikono yote Ili kuokoa uhai wake.

Akizungumza ofisini kwake Wilayani Kilosa, Mkuu wa Wilaya ya hiyo Shaka Hamdu Shaka amesema baada ya kupata changamoto ya kijana huyo serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itagharamia gharama za ununuzi
wa Viungo bandia Ili kimuwezesha kumudu majukumu yake ya kawaida hasa katika kufanya shuhuli ndogo ndogo za kujipatia kipato na kuweza kujikimu na familia yake.

“Inasikitisha sana na tunaendelea kulaani vikali vitendo hivi vya ukatili dhidi ya binadamu ambavyo vinadumaza shuhuli za mtu moja moja katika kupambania maisha, kitendo hiki kimeua ndoto za ndugu yetu hivyo Serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan itahakikisha tunamsaidia kupata viuongo hivyo bandia ili aweze kujisaidia” amesema Shaka.

Shaka ameleeza kuwa Serikali itaendelea kujali na kuhudumia wananchi wote wenye changamoto mbali mbali hivyo itamsaidia kijana huyo ili aweze kufanya shughuli ambazo zinaweza kumuingizia kipato kwa vile tayari anayo familia inayomtegemea kama baba.

“Gharama za viungo bandia pamoja na matibabu ni T. Shs, Milioni 15 tukumbuke hana mikono wote miwili na miguu yote miwili, niendelee kuwasili watanzania wenye moyo wa kumsaidia waendeleee kufanya hivyo kwani bado anahitaji msaada wa hali na Mali” amesema Shaka.

Kwa Upande wake Lucas Mhambo amesema tukio Hilo lilitokea Oktoba 14 mwaka 2023 baada ya mtu mmoja kuja eneo lake la kazi (bodaboda ) akiomba apelekwe Kijiji jirani, njiani waliongezeka na kumkaba kisha kumfunga kamba miguu ,mikono huku mdomoni wakimfunga kitambaa na kumtupa msituni ambapo alionekana na raia wema baada ya siku tatu kupita.

Amefahamisha kuwa baada ya Siku ya tatu kupita na wasamalia wema alifikishwa hospital kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini nilibanika viungo hivyo vimeharibika na haiwezi kutibika zaidi ya kukatwa vyote ambapo hadi sasa anaishi na ulemavu huo.

Hata hivyo Lucas amewashukuru watanzania wote waliojitolea kipindi chote cha matibabu yake akiwa hospital ya Taifa Muhimbili na akiwa nyumba ambapo michango hiyo imemuwezesha kufanya huduma za matibabu kuwa nyepesi na kuanzia kuanzia maisha.

“Namshukuru sana Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kuguswa na changamoto hizi kunishika mkono, watanzania wote waliojitolea kunisaidia mungu atawalipa zaidi walichotoa kwangu bado nahitaji msaada wao napitia magumu mno na kwa atakaeguswa anaweza kunisaidia kupitia Acc No 22710017881 Adam khalfa NMB Bank. Simu 0717382021” Amefafanua Lucas huku machozi yakimwagika.

Pamoja na kuwa serikali itamchangia matibabu na kununua viungo bandia imebainika kuwa na bado kijana Lucas anahitaji kununua kiti mwendo na kujenga nyumba ambayo amefikia hatua ya kupaua sambamba na changamoto ya fedha za kurejea hospitali kila baada ya siku Tano Ili kusafisha vidonda ambavyo anaendelea kujiuguza.