October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo yamshukuru Rais Samia kuwatatulia changamoto zao

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

JUMUIYA ya Wafanyabiashara Kariakoo hiyo imemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara na kutatua changamoto zao.

Pia imesema inatarajia kufanya Mkutano wake Mkuu Juni 13 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 07,2024 Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Martin Mbwana amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele kikubwa kwa wafanyabiashara nchini.

Amesema wameweza kukutana na Wizara zaidi ya tano ikiwemo Wizara ya Fedha na Wizara ya viwanda na Biashara na kufanya mazungumzo yanayochangia uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.

“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa busara hizo, Waziri wa Fedha tulikutana naye lakini kubwa tulijadiliana nae namna ya ulipaji wa kodi bila kuleta changamoto, tunataka ule ushirikishwaji na urahisi wa ulipaji kodi,” amesema.

“Lakini bado tunaumiza kichwa kuangalia ni namna gani utoaji wa risiti Kariakoo utakuwa mzuri bila kutumia nguvu kama ilivyo wenzetu wa mafuta na watumishi wa serikali ambao wanatoaga risiti bila matatizo yoyote,” amesema.

Ameongeza kuwa anategemea kupitia hotuba ya bajeti Waziri wa fedha ataainisha mambo ambayo wafanyabiashara wataweza kuyatumia katika matumizi ya risiti ya EFD.

“Tunawaomba TRA wanapotekeleza majukumu yao wasijifiche, tushirikiane Kwa pamoja tuijenge nchi yetu sote, wafanyabiashira tupo tayari kulipa kodi bila shuruti, Nipende kutoa wito kwa TRA hata wanapoleta vijana wapya katika kukusanya kodi watutambulishe wasinifiche wakawa wanawawinda wafanyabiashara,” amesema.