October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo aagiza bajaji na daladala kupangwa

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Mbozi

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe, kukutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ardhini (LATRA) ili kutengeneza mpangilio mzuri wa shughuli za usafirishaji abiria katika Miji ya Vwawa na Mlowo wilayani humo.

Agizo hilo amelitoa Juni 6, 2024 mara baada ya kutembelea na kukagua ukamilishaji wa stendi ya magari ya abiria ya Mlowo na kupokea malalamiko kutoka kwa madereva wa daladala akiwemo Daniel Mbusa ambao wamelalamikia bajaji kufanya shughuli zao bila mpangilio, hali ambayo imesababisha utendaji kazi wa daladala kuwa mgumu kati ya Miji ya Vwawa na Mlowo.

“Mkuu wa Wilaya naomba mkutane na LATRA kwa ajili ya kutengeneza utaratibu na uratibu mzuri wa shughuli za usafirishaji abiria ili kila mtu aweze kufanya kazi na kupata ridhiki,”ameagiza Chongolo.

Pia Chongolo ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Mbozi kuendelea kufanya maboresha ya miundombinu ndani ya stendi hiyo ikiwemo kuwekwa kokoto ili kuzuia vumbi, vihifadhia taka, taa, pamoja na mlinzi.

Vilevile, Chongolo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga kuhakikisha anasimamia magari yote ya abiria ili yafanye shughuli zake kwa kufuata taratibu kwa mujibu wa leseni zao, ikiwemo kuingia ndani ya stendi hiyo kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria na si vinginevyo.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Mbozi,Esther Mahawe amesema kuwa zoezi la uratibu wa wafanyabiashara kumalizia ujenzi wa vibanda hivyo unaendelea vizuri ambapo wamiliki wa vibanda 226 wamekubaliana kufikia maridhiano ya kuunganisha vibanda ambapo vyumba viwili vitatoa chumba kimoja ili kufanya mazingira ya ufanyaji biashara kuwa bora ndani ya stendi hiyo.

“Mkuu wa Mkoa sisi tunaendelea na utekelezaji wa maagizo yako na tayari wamiliki 226 wa vyumba wamekubaliakuachiana vyumba kama ulivyoshauri na wameahidi kuwa kuanzia kesho wanaanza kazi ya kumalizia ujenzi ili waanze kufanyabiashara, ingawa bado kuna wengine 30 tunaendelea nao, lakini kwa asilimia kubwa maagizo yako yametekelezwa,”ameeleza Mahawe.

Mei 14,2024 Mkuu huyo wa Mkoa Daniel Chongoloa alitembelea stendi hiyo na kukutana na wamiliki wa vyumba vya biashara na kushauri wamiliki hao kukaa pamoja na kukubaliana kuunganisha vibanda kutoka vibanda viwili kuwa kimoja baada ya vile vya awali kuonekana kuwa ni vidogo hali iliyolalamikiwa na wafanyabiashara hao.