Na Israel Mwaisaka,Timesmajira Online Rukwa
MAMLAKA ya maji mjini Namanyere NAUWASA imeutambulisha rasmi mradi wa upanuzi na uboreshaji wa maji Namanyere wenye thamani ya Tshs,mil.815
Akiutambulisha mradi huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NAUWASA Hamisi Honero amesema kuwa mradi huo umekwisha anza kutekelezwa baada ya mchakato wa kuwapata wazabuni mbalimbali.
Amedai kuwa katika kiasi hicho cha fedha cha mil.815 wao mpaka sasa wameshapata mil.700 na kuwa milioni 115 iliyobaki itaingia wakati wowote huku mradi huo ukiendelea kutekelezwa.
Honero amesema kuwa katika mradi huo kuna shughuli nyingi zinatarajiwa kufanyika ambazo ni kujenga tanki la maji lenye ujazo wa lita 100.000 litakalokuwa juu ya mnara wa mita 9,kujenga nyumba 5 za mitambo katika maeneo ya Mabatini,Misunkumilo,Majengo na Nakambili.
Kazi nyingingine ni ujenzi wa Chemba,uchimbaji wa visima vitatu,ununuzi wa mabomba yenye urefu wa km 15 kata zote,ununuzi wa pump 5,utafiti wa maji chini ya ardhi,usafishaji na upimaji wa wingi wa maji kwenye visima vilivyopo na ufufuaji wa miundombinu iliyopo (matanki na mtandao wa bomba)
Akizindua rasmi mradi huo Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali amewataka NAUWASA kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezeka vizuri ili fedha hizo ziwe na matokeo kwa Wananchi kwa kuhakikisha maji yanapatikana na kuondoa kero ya maji Mjini Namanyere.
Pia amewataka viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji wakiwemo Madiwani kuhakikisha wanaifuatilia miradi hiyo inayotekelezwa ikiwa ni pamoja na kuifahamu kiundani zaidi na kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi huo na kuzizitatua.
Aidha amewataka kuishirikisha ofisi yake kila changamoto inayojitokeza kwa haraka ili kupata ufumbuzi wake na kutaka kuona mradi huo unakamilika kwa wakati.
Katibu wa CCM wa Wilaya Nkasi Hassan Moshi Ntalika amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuwa ni jukumu kwa watendaji hao kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na viwango kama njia ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia ya kumtua mama ndoo kichwani.
Baadhi ya wananchi akiwemo Anord Kaunda waliitaka serikali kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa kwani kuna miradi mingi ya maji imefanyika lakini tija imekuwa ndogo sana kwa maana tatizo la maji limekua likiendelea.
Hata hivyo Chrispini Wikula amedai kuwa kama fedha hizo zitasimamiwa vizuri na watekelezaji wa mradi na wasimamizi kwa maana ya NAUWASA wakiutanguliza uzalendo mbele imani yao ni kuwa sasa watakwenda kuondokana na tatizo la maji.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa