November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Korogwe: mafunzo ya TAKUKURU yataondoa rushwa vituo vya afya

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga William Mwakilema amesema mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa watumishi wa umma, yatasaidia kujiepusha na mgongano wa maslahi, upendeleo, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa, na kutumia mali za umma kwa manufaa binafsi.

Ameyasema hayo Mei 27, 2024 wakati anafungua semina ya umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji wa huduma za afya ya msingi katika halmashauri mbili za Wilaya ya Korogwe kwa watumishi hao ngazi za zahanati na vituo vya afya.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema akizungumza na watumishi wa afya hawapo pichani

“Ni matarajio kuwa mtatumia misingi hii ya maadili kujiepusha na mgongano wa maslahi, upendeleo, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa, kutumia mali za umma kwa manufaa binafsi, na mwenendo usiofaa katika jamii ili kuimarisha uadilifu, uwajibikaji na uwazi ambazo ni sifa muhimu za kiongozi bora.

“Nitumie pia fursa hii kutoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Korogwe kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU inapopanga semina na mafunzo ya aina hii, ili lengo la kuimarisha maadili na Utawala Bora liweze kufikiwa” amesema Mwakilema.

Mwakilema amesema Huduma ya Afya ya Msingi ina nafasi muhimu sana katika mfumo wa utoaji huduma za afya nchini, na mara nyingi vituo vya afya ya msingi, zahanati na vituo vya afya ndiyo mahali ambapo wananchi wanaanzia kupata huduma ya tiba.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Victor Swella akizungumza kwenye semina ya watumishi wa afya. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema (kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Goodluck Mwangomango (kushoto)

Ambapo kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya, ambapo kwa mwaka 2023 zaidi ya asilimia 74 ya Watanzania wamepata huduma kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri za wilaya.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa maadili katika utoaji wa huduma za afya ya msingi, tunatarajia semina hii iimarishe ubora wa utoaji huduma tukianzia kwenye lugha inayotumika katika kuwasiliana na wateja wanufaika wa huduma za afya ili kuonesha na kuliishi lengo la kuimarisha dhana nzima ya maadili na kujiepusha na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma na usimamizi wa rasilimali katika Sekta ya Afya” amesema Mwakilema.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Victor Swella alisema wanafanya semina kwa watumishi wa Sekta ya Afya kwa ngazi ya zahanati na vituo vya afya kwa vile Serikali imeboresha kwa kiasi kikubwa miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba na dawa, lakini bado utoaji huduma ni mdogo.

“Lakini vile vile kama tunavyojua, watumishi hawa wanahusika na ukusanyaji wa zile fedha zinazotokana na uchangiaji wa huduma za afya katika vituo, kuna menejimenti yake ya namna ya kuziwasilisha na jinsi ya kuzitunza. Lakini vile vile na kikubwa zaidi, kuna miradi inaendelea, sasa kwa haya yote kama watumishi hawa hawataenenda kwa kufuata maadili bado ile nia njema ya Serikali ya kutaka kuweka huduma nzuri haitafikiwa” amesema Swella.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Goodluck Mwangomango akizungumza kwenye semina ya watumishi wa afya

Swella alisema mafunzo hayo kwa Mkoa wa Tanga yatatolewa kwa halmashauri zote 11 za mkoa huo. Nia ni kuona maadili yanafuatwa katika Sekta ya Afya, na huku vitendo vya rushwa ambavyo bado vipo kwenye sekta hiyo vinakwisha kama sii kupungua kabisa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Goodluck Mwangomango akizungumza kwenye semina hiyo, amesema TAKUKURU kwa sasa inafanya kazi kwa urafiki na watumishi wa umma, kwani tofauti na zamani ambapo walikuwa wanawawekea mitego watumishi ili wawakamate, sasa hivi wanawasaidia watumishi hao kujiepusha na mitego ya rushwa iliyopo mbele yao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Mwashabani Mrope akizungumza kwenye semina ya watumishi wa afya

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Mwashabani Mrope amesema semina hiyo itawaongezea nidhamu na maadili watumishi hao wa afya kwa kuhakikisha wanakuwepo kwenye vituo vya kazi kwa wakati muafaka, kwani wakati fulani ametembelea vituo vya kutolea huduma usiku kama raia wa kawaida, amekutana na mambo mengi ya ajabu kwenye baadhi ya vituo hivyo.

Washiriki wa Semina ya TAKUKURU kwa Sekta ya Afya