Na Ashura Jumapili, Timesmajira online,Bukoba
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajath Fatuma Mwassa,amesema ujenzi wa tawi la Chuo Kikuu cha Dar es -Salaam ( UDSM ) wilayani Bukoba mkoani humo kutasaidia kukuza uchumi na kuongeza viwango vya elimu kwa jamii .
Hajath Mwassa,amesema hayo wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi wa tawi la Chuo hicho katika Kijiji Itahwa Kata Kalabagaine Tarafa ya Kyamutwala kwa mkandarasi kwaajili ya kuanza ujenzi.
Amesema chuo hicho kimekuwa na manufaa ambayo ni fursa ya elimu kwa wananchi wa Kagera na nje ya nchi,kituo cha mafunzo ya ujasiriamali,kupanua mji na kuupendezesha.
Amewasaa wanafunzi kuhakikisha wanafikia elimu ya chuo kikuu kwa sababu elimu ya kidato cha sita haitoshi kikubwa ni kuwa na dhamira.
Amemtaka mkandarasi aliyekabidhiwa eneo kwaajili ya ujenzi kumaliza kazi kwa wakati.
Hata hivyo amesema mambo yanayotakiwa kufanywa na Mkoa katika miundombinu ya maji na barabara yafanyike haraka wasijekuwa kikwazo katika mradi huo muhimu.
Naye Makamu Mkuu wa UDSM Prof.Bonventure Rutinwa ,amesema kuwa mkataba unamtaka mkandarasi kumaliza kazi kwa muda wa miezi 18 tangu mkataba uliposainiwa Mei ,17 mwaka huu.
Prof.Rutinwa amesema gharama za awali za ujenzi ni zaidi ya bilioni 20 zitakazotumika katika mradi huo.
Amesema baada ya ujenzi kukamilika wataanza na kozi za masomo ya biashara uchumi wa kimataifa na kutakuwa na kituo cha mafunzo ya ujasiriamali ambacho kitafundisha kila mwananchi hata ambaye hakwenda shule ili waweze kuendesha shughuli zao.
Amesema eneo hilo lina ukubwa wa ekari 350 na limeshapatiwa hati miliki kwa kushirikiana na serikali ya Mkoa na halmashauri.
Amesema pia wataongeza kozi zingine baadae kadri itakavyohitajika ikiwemo tehama.
Johansen Rwehumbiza ,amesema ujio wa chuo hicho imekuwa fursa kubwa kwa wananchi kwa sababu watu watafanya biashara kutokana na uwepo wa chuo hicho na kujiongezea kipato.
Rwehumbiza,amesema ajira zitaongezeka kwa wananchi na watu wa eneo hilo watajifunza mambo mbalimbali kutoka kwa watu watakaofika katika chuo hicho.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa