November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA yatoa utabiri wake wa msimu wa Kipupwe

Na Penina Malundo, Timesmajira

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imesema  katika kipindi cha msimu wa Kipupwe(JJA) inatarajiwa  kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi katika maeneo mengi nchini.

TMA imetoa taarifa hiyo jana katika mwelekeo wa  hali ya joto, upepo na mvua katika msimu wa JJA inayotarajiwa kuanza Juni hadi Agosti mwaka huu imesema hali ya baridi ya wastani hadi kali unatarajiwa katika maeneo ya kusini mwa Morogoro,Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe

“Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza kati ya Julai mwaka huu ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 7  na nyuzi joto 15  na katika maeneo yenye miinuko kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 7,”imesema TMA.

Katika taarifa hiyo ilieleza kuwa mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo hayo ambapo  kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15  na nyuzi joto 20.

TMA imesema mikoa  ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo hayo kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 23 na 26 kwa maeneo ya mwambao wa Pwani na visiwani na kati ya nyuzi joto 17 na nyuzi joto 23 katika maeneo ya nchi kavu. 

Hata hivyo, maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 17. 

Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo hayo,  kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 na nyuzi joto  20 na maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 15.

Aidha TMA imeitaja mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 na nyuzi joto 20 huku maeneno ya kusini mwa mkoa wa Katavi yanatarajiwa kuwa na  baridi ya wastani hadi baridi kali chini ya nyuzi joto 15.

 Kanda ya kati mikoa ya Singida na Dodoma hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 11 na nyuzi joto 17

TMA imesema  ukanda wa Pwani ya kusini mkoa ya Mtwara na Lindi hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 17  na nyuzi joto 22

Kwa upande wa mwenendo wa upepo TMA imesema msimu wa Kipupwe hutawaliwa na upepo wa kusi ambapo unatarajiwa kuwa wa wastani hadi upepo mkali utakaovuma kutoka kusini mashariki na vipindi vichache vya upepo wa kusi katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

TMA imesema katika  kipindi cha msimu wa Kipupwe  kinatawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi hata hivyo vipindi vichache vya mvua vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Simiyu na Mara, kaskazini mwa  Kigoma, Arusha na Kilimanjaro pamoja na  Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

Katika mifumo ya hali ya hewa katika kipindi cha msimu huo hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuwa ya wastani hadi chini ya wastani ikiashiria kuelekea hali ya La Nina mwishoni mwa msimu hali hiyo inatarajiwa kuwa na mchango hafifu katika mifumo ya mvua hapa nchini.

TMA imesema Bahari ya Hindi, joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa kuendelea kuwepo katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Afrika Mashariki) ikilinganishwa na joto la Bahari upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Indonesia).

 “Hali hiyo inatarajiwa kuimarisha mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo jirani,

“Upepo unatarajiwa kuvuma kutoka misitu ya Kongo kuelekea nchini hali hiyo inatarajiwa kuimarisha mifumo inayosababisha mvua hasa katika maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na ukanda wa Ziwa Viktoria,”imesema 

Pia vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kusababisha  magonjwa mbalimbali ikiwemo  ya macho.