Juditha Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) inatarajia kutekeleza mradi wa miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira utakaonufaisha wananchi 7,300 sawa na Kaya 1,600 kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria.
Mradi huo unafadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya Ujerumani(KfW) na Umoja wa Ulaya (EU) chini ya uratibu wa LVBC kupitia programu ya Pamoja ya Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria (LVB-IWRM).
Hayo yameelezwa Mei 26, 2024 jijini Mwanza katika kikao kilichoshirikisha wadau kutoka MWAUWASA, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) ukiongozwa na Mkurugenzi wa benki Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Christoph Tiskens
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA,Neli Msuya amesema dhamira ya mradi ni kuhakikisha mazingira katika Ziwa Victoria yanahifadhiwa kwa kuwa na mfumo rafiki wa uondoshaji majitaka hususani katika maeneo ya miinuko.
“Mradi utawezesha ukarabati na upanuzi wa mtandao wa majitaka kwa takribani Kilomita 14.4 sambamba na ukarabati wa miundombinu ya majitaka, uboreshaji vituo vya kusukuma majitaka na ununuzi wa vifaa vya usimamizi wa mfumo huo yakiwemo magari ya kuondoa majitaka nyumbani mbani,”ameeleza Neli.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Neli, ni kwamba kaya zipatazo 1,600 zitanufaika kutoka katika maeneo ya Pasiansi, Kitangiri, Nyamanoro, Kirumba na Igogo.
Mara baada ya kikao, wajumbe wakiongozwa na Mkurugenzi wa MWAUWASA Neli na wataalam wa miradi wa mamlaka hiyo walioambatana nao walipata fursa ya kutembelea mnyororo wa uondoshaji majitaka kwa wanufaika wa eneo la Pasiansi sambamba na kuzungumza na baadhi ya wanufaika, mabwawa ya majitaka-Butuja na Kituo cha kusukuma majitaka Mjini Kati.
Mkurugenzi wa KFW, Christoph Tiskens amepongeza hatua zote alizoshuhudia za miradi iliyotekezwa hapo awali na amrthibitisha kuwa taasisi yake itaendelea kufanya kazi na MWAUWASA huku pia akipongeza ushirikiano uliopo baina ya mamlaka hiyo na LVBC.
“Nimeridhishwa na nilichokishuhudia, nimejionea dhamira ya dhati mlionayo katika suala hili la utunzaji wa mazingira. Nimeona namna ambavyo wananchi wananufaika, kwa pamoja tutahakikusha mradi hui unafanikiwa,” amesema Tiskens.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili