Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Magu
WANANCHI wa Vijiji Bugando, Nyashigwe,Chabula na Kongolo wilayani Magu,mkoani hapa wameondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama baada serikali kukamilisha mradi wa maji Chabula-Bugando kwa gharama ya bilioni 1.78.
Mradi huo ambao chanzo chake ni Ziwa Victoria,umetekelezwa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)ikishirikiana na MWAUWASA,utawanufaisha wananchi 12,400 wa vijiji hivyo.
Wakizungumza leo mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza,baadhi ya akinamama wa vijiji hivyo wamesema, mradi huo umewaondolea adha ya muda mrefu ya ukosefu wa majisafi na salama.
“Tunamshukuru sana Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa fikra nzuri za kutuletea huduma ya maji, kwa umri wangu huu siwezi kuteka maji umbali mrefu, hivyo mradi huu umtuondolea shida tuliyokuwa tukiipata,”amesema Martha Kayungilo.
Naye Joyce Edward amesema; “Tunamshukuru mwanamke mwenzetu kwa kusikia kilio chetu na kuamua kutuletea maji hadi nyumbani kwani suala la maji ilikuwa changamoto kubwa katika vijiji vyetu,”.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM, Israel Mtambalike,amesema akiana mama kiuchumi ni wazalishaji wakubwa hivyo kwa mradi huu sasa watazalisha zaidi baada ya kuondokana na adha ya maji.
“Matokeo haya makubwa yako ndani ya CCM na lengo ni kumtua mama ndoo kichwani,rai yangu sasa utunzeni mradi uwe endelevu uendelee kuwanufaisha na atakaye uharibu mkeemeni,”amesema Mtambalike na kushauri RUWASA kuongeza idadi ya vituo vya kuchotea maji.
Aidha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ amesema ziara hiyo ya kamati ya siasa inalenga kubaini matumizi sahihi ya fedha za serikali za miradi ya maendeleo.
“Tumekuja kumwakilisha Rais Dk.Samia kuona hizo sh. bilioni 1.7 zimefanya nini kwa ajili ya wananchi, tumeridhika na mradi huu mkubwa umetekelezwa kwa viwango na thamani ya fedha inaonekana, hivyo endeleeni kuiunga mkono serikali na Rais wetu kwa maono na kazi nzuri anayoifanya ya kuleta maendeleo,”amesema.
Awali Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Magu, Mhandisi Daud Amlima ameiambia kamati ya siasa kuwa mradi wa maji Chabula-Bugando umekamilika kwa asilimia 100 na unahudumia vijiji vinne vya Chabula, Bugando, Nyashigwe na Kongolo na unatoa huduma nzuri kupitia vituo 31 vya kuchotea maji.
Amesema maeneo ambayo hayakufikiwa na mradi kwa kuwa hayakuwa katika usanifu wa awali,wamekamilisha kujenga DP 1 katika Kitongoji cha Dihu katika Kijiji cha Bugando na hivyo kufikisha jumla ya vituo 32 vya kuchotea maji.
Katika hatua nyingine Kamati ya Saisa ya Mkoa imeridhishwa na ubora wa nyumba pacha ya watumishi wa Zahanati ya Kijiji cha Bugando iliyogharimu sh.milioni 103.5 za Mfuko wa TASAF, kati ya fedha hizo jamii iliichangia nguvu zao sawa na sh. milioni 11.09.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Fransisca Msoga,amesema nyumba hiyo ya watumishi itawawezesha jamii kuhudumiwa na wataalamu hao wa afya kwa karibu zaidi wakati wote.
“Kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Bugando,tunaishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya afya wananchi wapate huduma bora na kukidhi matakwa ya Malengo Endelevu (SDGs) 2030, na ilani ya Uchaguzi ya CCM ibara ya 83 (d) na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025,”amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ amesema serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa mujibu wa ilani yake, hivyo juhudi za wananchi kushiriki ujenzi wa nyumba ya watumishi utawawezesha kuhudumiwa kwa karibu.
“Tumekuja kuona namna serikali inavyopambana kuimarisha huduma za jamii katika sekta za afya, maji na elimu, tunawapongeza na kuipongeza kwa kazi hii nzuri ilinayolingana na thamani ya fedha,”amesema.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi