November 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yataka viongozi Kwimba kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Kwimba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mwanza kimeitaka Serikali wilayani Kwimba kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi ya maendeleo ukiwemo wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya hiyo ikamilike kwa wakati kulingana na thamani ya fedha.

Pia kimeridhishwa na matumizi ya fedha na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo kwa fedha za mapato ya ndani na Serikali Kuu.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza,Michael Masanja ‘Smart’ ameagiza leo, baada ya Kamati ya Siasa kukagua miradi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya hiyo.

“Naipongeza halmashauri ya Kwimba imetekeleza miradi kwa viwango na thamani ya fedha inaonekana, imeonesha jinsi gani ilani ya CCM imetekelezwa kwa kasi zaidi katika sekta za afya, utawala na elimu.DC (Mkuu wa Wilaya niendelee kuwapongeza kwa kubwa na nzuri lakini ongezeni kasi ya usamamizi kwani kazi iliyobaki ina gharama kubwa,”amesema.

Wajumbe wa Kamati hiyo ya Siasa,Israel Mtambalike na Mwenyekiti wa Wazazi, Mohamed Lukonge kwa nyakati tofauti wameshauri uadilidifu na ubora wa usimamizi katika miradi.

“Uongozi wa pamoja na umoja uliopo, ongezeni ubora na usimamizi matokeo ya kuvunja mkataba na mkandarasi yaonekane kwa kuwatumia wataalamu wa ndani,”amesema Mtambalike.

“Mradi hu unajieleza wazi na niwapongeze,wengine fedha zinapoletwa hazitekelezi miradi hadi zinarudishwa, tunawapongeza kwa ujasiri wa kuvunja mikataba.Hizo bilioni 1.7 zitumieni kwa uaminifu thamani yake ionekane,”amesema Lukonge.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kwimba (DED), Happiness Msanga,amesema kasi ndogo ya mkadarasi wa jengo la utawala linalogharimu bilioni 3.4,ilisababisha wavunje mkataba na kuwatumia wataalam wa ndani katika ujenzi huo.

“Kati ya sh.bilioni 3.4 awamu ya kwanza tulipokea bilioni 1.7 na awamu ya pili milioni 400, hivyo katika mwaka huu wa fedha 2024/25 mradi huo utakamilika na kuwezesha watumishi kuwadumia wananchi wakiwa eneo moja badala ya kutawanyika,”amesema.

Msanga amesema mradi huo unaotekelezwa eneo la Iteja ulianzishwa sababu ya jengo ya zamani kutokutosheleza na kusababisha watumishi kugawanyika,hivyo likikamilika litarahisisha utoaji wa huduma kwa watumishi kufanya kazi eneo moja.

Kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo uliogharimu zaidi ya sh. bilioni 3 kati ya fedha hizo,wameshapokea sh. bilioni 1.39,baadhi ya miundombinu imekamilika na imeanza kuhudumia wananchi.

“Faida za kujenga hospitali hii ni pamoja na wagonjwa kutambua umuhimu wa kupata huduma za matibabu,huduma zimeongezeka,vifaa tiba vya kisasa vya sh. milioni 375 vimenunuliwa,”ameeleza Msanga.

Mkurugenzi huyo Mtendaji amesema pia,mapato kwa mwezi yameongezeka kutoka sh.milioni 4 hadi sh milioni 13 baada ya kupata majengo mapya,wanahudumia wagonjwa 450 hadi 700 kutoka wagonjwa 300 kwa siku,wagonjwa wa kliniki 1200 hadi 1500 kutoka 400 hadi 700 waliokuwa wakihudumiwa katika majengo ya zamani.