Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Sengerema
HALMASHAURI ya Wilaya ya Sengerema imepongezwa kwa ubunifu wa ujenzi wa uwanja wa michezo wilayani humo kuwa utachochea ukuaji wa michezo na mapato ya halmashauri hiyo.
Pongezi hizo zilitolewa leo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart ‘ kwa niaba ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa, baada ya kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wilayani Sengerema.
“Kamati tunapongeza kwa mradi huu wa uwanja unaokidhi mahitaji ya wananchi wa Sengerema na halmashuri mtakusanya mapato sahihi kupitia michezo, pia ukikamilika mengi yatafanyika ambapo timu kubwa za Simba, Yanga na Pamba zitakuja kucheza hapa,”amesema Smart.
Amesema uwanja wa michezo Mnadani lilikuwa hitaji la wananchi muda mrefu ,hivyo serikali na uongozi wa halmashauri umeridhia ujenzi huo kwa mapato ya ndani.
Amewahimiza wananchi kuchapa kazi n kueleza kuwa serikali itaendelea kuleta fedha za miradi ya maendeleo wafaidi matunda ya kodi zao.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema serikali ni kuona mradi huo ukikamilika utasaidia kuinua michezo na mapato ya Sengerema.
“Timu ya Pamba itaweka kambi hapa pia nitamleta Diamond kuufungua rasmi, hivyo fanyeni hima mradi ukishakamilika nitaileta Pamba na Yanga hapa,Sengerema mtapata mapato hapa Mnadani,”amesema.
Awali Ofisa Uchumi na Mipango wa Halmashauri ya Sengerema, Wilbad Bandola amesema lengo la kujenga uwanja wa michezo Mnadani ni maelekezo ya Ilani ya CCM, utasaidia kuibua na kukuza vipaji na kuendeleza michezo .
Mbali na kuinua sekta ya michezo pia, uwanja huo utasaidia kuongeza mapato ya halmashauri kwa viingilio vya milangoni na vibanda vya biashara vitakavyojengwa kuzunguka uwanja.
“Fedha za gharama za ujenzi ni milioni 361.2 za mapato ya ndani, mfuko wa jimbo, ufadhili wa mbunge na wadau wa maendeleo,awamu ya kwanza ya ujenzi utahusisha uzio na miundombinu mbalimbali , ukikamilika utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 15,000 hadi 20,000 kwa wakati mmoja,”amesema Bandola.
Amesema miundombinu inayoendelea kujengwa ni uzio (ukuta), matundu 24 ya vyoo hadi sasa sh. milioni 220.5 zimepokelewa kati ya sh.milioni 361.2 na zilizokwisha kutumika kwa ujenzi huo ni sh.milioni 189.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi