November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Muhongo aiomba serikali ijenge viwanda Mara

Fresha Kinasa, TimesMajira Online,Mara.

SEREKALI imeombwa kujenga Viwanda 10 katika Mkoa wa Mara ili kuufungua Mkoa huo kiuchumi kutokana na uwepo wa shughuli za kilimo,ufugaji na uvuvi ambazo zinamchango katika kuchochea maendeleo kwa wananchi pamoja na kuzalisha fursa za ajira.

Kauli hiyo imetolewa Mei 21, 2024 Bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijni Prof. Sospeter Muhongo wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara huku akiwaomba wabunge kupitisha bajeti ya Wizara hiyo licha ya madai yake kuwa ni ndogo.

“Kwa sasa Mkoa wa Mara hatuna kiwanda hata kimoja, ombi namba moja kama tuko kwenye mapinduzi ya viwanda mahali pa kuweka viwanda ni Mkoa wa Mara,kwani una wakulima bingwa wa pamba,tunaomba viwanda vipya vitatu vifanye kazi, tunaomba kiwanda kipya cha nguo,”amesema Prof. Muhongo na kuongeza kuwa;

“Sisi ni wavuvi wa samaki, kilichopo kinafanya kazi chini ya asilimia 15 tunaomba angalau vitatu, pia sisi ni wafugaji bingwa,tunaomba viwanda vya samaki vipya,”.

Prof. Muhongo amesema kuwa uwepo wa viwanda ndani ya Mkoa huo kutachochea kasi ya maendeleo mkoani humo huku akisema miaka ya 1960 hadi miaka ya 1990 Mkoa wa Mara ulikuwa na viwanda vingi lakini kwa sasa havipo,”.

Aidha ameomba maeneo matatu yaliyokuwa yakifanyika uchambuaji wa pamba yafunguliwe ili shughuli ziweze kuendelea tofauti na ilivyo sasa.

Huku akisema, Mkoa huo unahitajika kiwanda kipya cha nguo kwani mashine zilizopo kiwanda cha nguo cha Musoma (MUTEX)ni za zamani na spea zake hazipatikani.

Pamoja na kwamba miaka ya nyuma kulikuwepo na viwanda vya maziwa lakini navyo havipo licha ya Mkoa huo kuwa na idadi kubwa ya mifugo.

Pia, Prof. Muhongo ametoa historia ya mradi wa Liganga (chuma) na Mchuchuma (makaa ya mawe) na kuishauri serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa mradi huo kutokana na umuhimu wake.

Pastory Juma ni Mkazi wa Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma amesema kuwa, maendeleo ya Mkoa wa Mara yatapiga hatua iwapo viwanda vitajengwa kwa wingi, akitolea mfano vijana wengi kwa sasa hawana ajira lakini viwanda vikijengwa vitatoa ajira na hivyo kuwapa uhakika wa kipato.

“Mara hatuna Viwanda, tungekuwa na viwanda Mkoa ungekuwa na maendeleo makubwa, Niiombe serikali licha ya kufanya kazi nzuri kujenga miradi mikubwa pia ijenge viwanda,Mara ndiko alipozaliwa Baba wa taifa lakini hatuna Viwanda vya kumuenzi karibuni vyote vimekufa.” amesema Rhoda Juma mkazi wa Mtaa wa Songe Kata ya Bweri .