Na Edward Paul, Timesmajiraonline
WIKI iliyopita (Mei 14) Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa mwenyekiti mwenye katika mkutano wa nishati safi ya kupikia kwa Afrika uliofanyika nchini jijini Paris, Ufaransa.
Mkutano huo umekuwa ni fursa ya kuokoa vifo vya mamilioni ya watu, kupunguza upotevu wa viumbe hai, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ukuaji wa uchumi.
Rais Samia ameshiriki na kuwa mmoja wa wenyeviti wenza, huku takwimu za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), zikionesha kuwa kila mwaka watu milioni 3.2 wanakadiriwa wanakufa kutokana na moto wa moshi unaozalishwa na nishati zisizo safi kupikia.
Hiyo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus. Anasema robo ya idadi ya watu duniani inaathiriwa na moshi wa mkaa, kuni na mabaki ya mazao kama vyanzo vya nishati. Wanawake na watoto katika jamii masikini ndio waathirika wakubwa,” amesema Adesina.
Hivyo, Rais Samia aliakwa kushiriki mkutano huo kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuifanya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kimataifa. Rais Samia alialikwa na Dkt. Fatih Birol, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati (IEA).
Viongozi hao walikuwa wenyeviti wenza katika mkutano huo. Wengine walioshiriki mkutano huo ni Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre, na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina.
Mwaliko kwa Rais Samia ulitokana na mchango wake katika kutambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuweka msukumu katika kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kupikia na athari zake.
Zaidi ni kulinda mazingira ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo ulilenga kulifanya suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia kuwa la kipaumbele katika ajenda ya kimataifa.
Pia kuainisha mabadiliko madhubuti ya kisera yatakayoharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, na kutoa fursa ya washiriki kutoa ahadi za kifedha, sera na ubia ili kufikia azma ya kukuza matumizi ya nishati safi.
Mkutano huo ulijumuisha watu zaidi ya 900 wakiwemo wakuu wa nchi, taasisi na kampuni za kimataifa zinazohusika na nishati safi ya kupikia.
Akihutubia katika mkutano huo uliofanyika makao makuu ya UNESCO Jijini Paris nchini Ufaransa Mei 14, 2024,Rais Samia alitaja vikwazo vinakwamisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, ikiwamo gharama kubwa za vyanzo vya nishati.
Kikwazo kijingine ni mataifa tajiri kutotoa kipaumbele kwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na kutoshirikishwa kwa wadau wakiwamo wa teknolojia za kuzalisha nishati hiyo.
Nyingine gharama ya upatikanaji nishati hiyo vijijini ikilinganishwa na kipato chao. “Inasemwa kuwa nishati safi ya kupikia kidunia inapatikana kwa asilimia sita kusini na kati ya Asia na zaidi ya asilimia 14 kwa Amerika ya Kusini na Caribbean.
“Kinyume chake kwa Afrika ambayo ni bara lenye idadi kubwa ya watu na lenye rasilimali zote muhimu, ina kiwango cha chini cha kuwa na nishati hiyo,” anasema Rais Samia.
Anasema zaidi ya Waafrika 900 wanategemea nishati chafu, suala linalochangia uharibifu wa mazingira na upotevu bioanuai. “Familia nyingi zinapambana kupata nishati safi ya kupikia kutokana na gharama kubwa, kutopatikana kwake na ugavi ulio wa chini.
“Sababu ya pili ni ulimwengu kutotoa kipambele katika utoaji wa fedha za kutosha na kutojali kuwepo kwa fursa za kiuchumi katika uzalishaji wa nishati safi ya kupikia,” anasema Rais Samia.
Anataja sababu ya tatu kuwa ni kukosekana kwa ushirikishwaji ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya kupikia kwa wote. Katika kupambana na changamoto hizo, Rais Samia amesema Tanzania imeanzisha programu ya miaka 10 wa nishati safi ya kupikia, inayolenga kuhakikisha asiliamia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Kuhusu mzigo walionao wanawake katika kutafuta nishati safi, anasema Tanzania inahamasisha wanawake, sio tu kutatua changamoto za mazingira na magonjwa, bali pia kuwawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii.
Anaendelea kutaja mikakati mingine kuwa ni kuendelea kulinda mazingira kwa kuhakikisha mpango ya maendeleo inahusisha vijana kufikia nishati safi ya kupikia.
“Kuongezeka kwa fursa kutawawezesha wanawake kuwapa fursa za uzalishaji kiuchumi na kupambana na vichocheo vya umasikini na kutokuwa na usawa.
“Kwa upande mwingine, kupunguza matumizi ya kuni kama nishati inayotoa moshi wenye sumu kutaokoa maisha na tunaamini hilo litafanikiwa,” anasema Rais Samia.
Amesema Tanzania inajifunza kwa nchi za Brazil, India na Indonesia na Ghana zilizoweka mikakati ya kupata nishati safi.
“Ninapotazama picha ya Afrika, naona baada ya kazi ya hatari ya kupika na kupata moshi, ni kazi ya mwanamke kumlinda mtoto aliyembeba mgongoni ili asipate moshi,” anasema Gahr Store.
Anazitaka nchi wahisani, mashirika na asasi za kiraia kuungana kuchangia upatikanaji wa nishati safi. “Tuliungana ili kupata chanjo miaka 25 iliyopita na tulisaidia kupunguza vifo vya wanawake na watoto waliokuwa wakifa kwa magonjwa, hivyo sasa tunapaswa kutumia mkakati kama huo,” anasema Gahr Store.
Amesema wamekuwa wakisaidia miradi ya nishati nchi za Uganda, Tanzania, Ethiopia na Msumbji kupitia Benki ya Dunia, AFDB na asasi za kiraia.
“Ninayofuraha kutangaza leo kwamba Norway itawekeza Dola 50 milioni katika mpango huu. Tuko tayari kuendelea kusaidia mipango huu,” amesema Gahr Store.
Rais wa AfDB, Akinwumi Adesina amesema kuna wanawake bilioni mbili duniani ambao hawapati nishati safi ya kupikia wakitegemea kuni na mkaa kupikia. “Hawa wanawake hufanya kazi ngumu ya kupika huku wasichana wakikusanya kuni wakitembea kilometa nyingi ili kuhakikisha wanatayarisha chakula cha familia.
“Afrika inapoteza wanawake na watoto 600,000 kila mwaka kutokana na moto wa kuni na mkaa. Kama hatutabadilika watapotea wanawake na watoto milioni sita kwa miaka 10, hili halikubaliki,” amesema Adesina.
Amesema iwapo nishati safi itapatikana itawezesha kuokoa angalau hekta 200 milioni za misitu duniani kote ikiwamo Afrika.
Amezitaka nchi za Afrika kutenga angalau asilimia 5 ya Dola 7 bilioni (Sh17.53 trilioni) zinazowekezwa kila mwaka kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi barani humo.
“Hivyo ninayo furaha kutangaza kuwa AfDB itatoa Dola 2 bilioni (Sh5.01 trilioni) kwa ajili ya nishati safi ya kupikia kwa miaka 10 ijayo,” anasema Adesina.
***Hapa nyumbani
Kwa hapa nyumbani Tanzania, Rais Samia amevalia njuga suala la nishati safi ya kupikia akitaka Wizara ya Nishati kuongeza haraka upatikanaji wake kwa gharama himilivu.
“Kaeni na wizara muone wapi tubane, wapi tuongeze na wapi tupunguze ili tuweke bei himilivu na wananchi wengi zaidi watumie (Nishati safi),” anasema Rais Samia.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati akizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam Mei 8, 2024.
Anahimizwa kuwekwa mazingira wezeshi ya upatikanaji wake, kwa kupunguza bei na kuongeza wingi madukani.
Anataka Wizara ya Nishati jukumu hilo na Serikali kuu itabeba jukumu la utoaji elimu na kutunga sera wezeshi.
“Jukumu la Serikali ni kutunga sera wezeshi kufikia malengo ya mkakati na kutoa elimu kwa wananchi, huku Wizara ya Nishati ikiwa na jukumu la kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa uhakika na bei himilivu,” anasema Rais Samia.
Kwa sasa uamuzi ambao Tanzania inakwenda nao ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 3034, miaka kumi ijayo?
***Je tunafikaje huko?
Akitangaza safari ya kufikia lengo hilo, Rais Samia alitoa agizo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ndani ya miezi mitatu ifikapo Afosti, mwaka huu liwe limeandaliwa katazo kwa taasisi zinazohudumia watu kuanzia 100 kuacha kutumia kuni na mkaa.
Hatua hiyo ya Rais Samia analenga kile alichoeleza, kuzishinikiza taasisi hizo zihamie kwenye matumizi ya nishati safi. Hata hivyo, marufuku ya Rais Samia inakuja katika kipindi ambacho kati ya magereza 126 zilizopo nchini, 76 zinatumia nishatisafi ya kupikia.
Sambamba na magereza, kati ya vyuo vya elimu 35 vilivyopo 30 zinatumia nishati safi kwa ajili ya kupikia.
Kutokana na hatua iliyofikiwa na taasisi hizo, Rais Samia amesema: “(Dk Jafo) andaa katazo taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 ni marufuku kutumia kuni na mkaa, ukipiga katazo wataingia.” Ili kutekeleza mkakati huo, ametaka wadau wote muhimu wafikishiwe kwa njia rasmi, uwekwe kwenye tovuti ya wizara ya nishati na utafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Rais Samia ametaka kutungwa sheria itakayounda mfuko wa kuendeleza nishati safi ya kupikia kufikia mwaka 2025, akisisitiza Serikali itatafuta namna ya kuujazia. Katika kuujaza mfuko huo, aliahidi kuendelea kutumia majukwaa mbalimbali ya kimataifa ili kuzishawishi nchi zilizoendelea zitekeleze ahadi ya kutoa fedha kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameeleza fedha hizo zitakazotolewa, pamoja na mambo mengine zitatumika katika utekelezaji wa mkakati huo.
Anataka wakuu wa mikoa waongezewe kipengele cha matumizi ya nishati safi kama mmoja ya vigezo vya kupima utendaji wao.
Anawataka wakuu wa mikoa kuwafikia wadau na kuwatambua ili wafikishe nishati hizo katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kuna haja ya nishati safi kuingizwa katika dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050, huku Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ikitakiwa kujipanga ili kutekeleza majukumu yake yaliyopo katika mkakati huo.
Katika utekelezaji wa nishati safi ya kupikia, ametaka sekta binafsi ije na mbinu kuleta teknolojia rahisi ya matumizi ya nishati akitolea mfano wa kulipia kwa kadri
***Athari za kutotumia nishati safi ya kupikia
Kwa mujibu wa Rais Samia hekta 469,000 za misitu zinakatwa kila mwaka na nishati za kuni na mkaa ni moja ya chanzo kikuu cha hayo. Kwa kadri misitu inavyopotea, amesema utafika wakati hata upatikanaji wa nishati ya kuni na mkaa utakuwa mgumu na hivyo kuwafanya wananchi watumie muda mwingi kutafuta nishati kuliko chakula.
“Yaani kutafuta chakula ni rahisi kuliko kwenda kutafuta chakula chenyewe,” anasema.
Awali, akizungumzia mkakati huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kazi ya maandalizi yake ilitekelezwa na kamati ya kitaifa inayojumuisha wizara, idara, wakala na wataalamu kutoka taasisi za elimu, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi. Amesema uundaji wa kamati hiyo ulizingatia kuhakikisha ushiriki wa wadau wote muhimu katika utayarishaji wake wanashirikishwa.
Kwa mujibu wa Majaliwa, kamati hiyo pia inajumuisha pande mbili za muungano yaani Bara na Zanzibar.
Majaliwa amesema mkakati huo umezingatia masuala ya kisera, miongozo na kanuni zinazosimamia utendaji yatakayosaidia kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa. Mambo mengine amesema ni kuondoa vikwazo vya uendelezaji nishati safi ya kupikia na uratibu wa namna bora ya kushirikisha wadau katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia.
Ameeleza mkakati huo dhima yake ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi na nafuu Amesema wanaoanisha sera, sheria, kanuni na miongozo ili iwe wezeshi kwa wote wanaoanza kutoa huduma ya nishati safi ili iwe rahisi kwa kila mmoja kuipata.
Dira yake ni kila Mtanzania atumie nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao. Kwa mujibu wa Majaliwa, mkakati huo utagharimu sh. trilioni 4.6 na kwamba utekelezwaji wake utahusisha wadau wote.
Kwa upande wa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema atahakikisha mkakati unaozinduliwa hauishii kuonekana kwa kupigwa picha, badala yake unazaa matunda tarajiwa.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Rais Samia, ameibeba kwa dhati ajenda ya matumizi ya nishati mbadala kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
“Ninyi nyote mnafahamu ajenda ya Rais kuhusiana na umuhimu wa nishati mbadala, tunafahamu changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za mazingira kwa ujumla. Hii ni ajenda ambayo Mhe. Rais ameibeba kwa dhati kabisa kuhakikisha tunaanza mchakato wa kuelimisha Watanzania ili kuondokana na nishati ambazo sio rafiki kwa mazingira, na kutumia zilizo rafiki kwa mazingira,” amesema Mhe. Kapinga.
Naibu Waziri Kapinga ambaye pia ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma anawataka vijana kushirikiana na wanawake, wazee na makundi mengine katika kuhakikisha wanapunguza changamoto za kimazingira kwa matumizi ya nishati mbadala.
“Wengi wanadhani ajenda hii ya nishati mbadala ni kwa ajili ya akina mama tu, lakini wote tunafahamu nguvu na mchango wa vijana kwenye masuala ya mabadiliko chanya. Kwa hiyo ajenda hii ni lazima twende nayo pamoja wanawake, vijana, wazee na kila kundi kwenye jamii. Ndiyo maana nikaona busara kushirikisha Baraza la Mkoa kwa sababu ninyi ndio viongozi kwenye Wilaya zenu,” anasema Kapinga.
Akifafanua, anasema kuwa ajenda ya matumizi ya nishati mbadala ni ya Serikali ya Awamu ya Sita na inatakiwa kuungwa mkono na wananchi wote ili kuweza kuboresha mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea hivi sasa duniani kote.
Kapinga anasema ni wakati wa vijana kusaidia katika anjenda mbalimbali zenye manufaa ya taifa na kwamba ajenda ya nishati mbadala ikibebwa na vijana inaweza kwenda kwa kasi katika kusaidia kupunguza changamoto za uharibifu wa mazingira unaofanywa na jamii.
Aidha, anaongeza kuwa wakati huu ambapo REA wanaendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati mbadala, Mhe. Rais ametoa mitungi ya gesi kwa Wabunge wote ili iende kwenye maeneo yote, na majimbo yote ili kuhamasisha umuhimu wa nishati mbadala.
Awali, akiwasilisha mada kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhandisi Kelvin Tarimo kutoka REA amesema Wakala hiyo inaendeshwa kwa Mipango Mikuu mitatu ambayo ni Mpango wa Sera ya Taifa wa Upelekaji Nishati Vijijini (Rural Energy Master Plan), Mpango wa usambazaji wa huduma ya umeme vijijini (Rural Electrification Master Plan) pamoja na Mpango wa Nishati safi za kupikia.
Kuhusu Mpango wa nishati safi ya kupikia, Mhandisi Tarimo amesema umelenga kuhamasisha matumizi ya nishati iliyo salama kwa mtumiaji na kwa mazingira, ubora, upatikanaji wake, gharama nafuu, rafiki kwa mazingira na iliyo endelevu.
Akizungumzia aina za nishati za kupikia na kiwango cha matumizi yake kwa hapa nchini, Mhandisi Tarimo amebainisha kuwa kuni inaongoza kwa asilimia 63. 5 ikifuatiwa na mkaa asilimia 26.2, gesi oevu asilimia 5.1, umeme asilimia 3 na asilimia 2.2 vyanzo vinginevyo.
Anasema, kutokana na matumizi makubwa ya mkaa na kuni, imechangia uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na ukataji miti. Pia, amesema athari nyingine ni za kiafya kwa watumiaji wa nishati hizo ambapo vifo zaidi ya 33,000 hutokea kwa mwaka kutokana na kuvuta hewa ya ukaa. Vilevile, kiuchumi amesema matumizi ya nishati zisizo salama yanachelewesha maendeleo ya shughuli za kiuchumi.
Kufuatia hali hiyo, amesema Serikali imeweka mikakati ya makusudi katika kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala hivyo akatoa wito kwa wananchi wanaopata elimu hiyo kuifikisha kwa wengine.
Amewasihi wananchi kubadili mitazamo hasi dhidi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo imani kwa baadhi ya watu kwamba chakula huwa kitamu zaidi kikipikwa kwa kutumia mkaa au kuni kuliko kikipikwa katika jiko la gesi au umeme.
Mhandisi Tarimo ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika