Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),Mohamed Salum, amesema wanachunguza chanzo cha kupinduka na kuzama kwa Meli ya MV. Clarias tukio lililotokea usiku wa kuamkia Mei 19, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza,Mei 21, mwaka huu baada ya kutembelea eneo la ajali,amesema wameanza uchunguzi wa kitalaam wa kubaini sababu na chanzo cha MV.Clarias kupinduka na kuzama majini ndani ya Ziwa Victoria.
“Baada ya kutembelea eneo la tukio tumeanza uchunguzi wa kitaalamu kubaini kilichosababisha meli kulalia upande mmoja kabla ya kuzama majini ikiwa imetia nanga Bandari ya Mwanza Kaskazini, tutazungumza na wafanyakazi (nahodha na mabaharia),kufahamu meli ilikuwa na changamoto gani watusaidie kabla ya uchunguzi utakaohusisha chombo chenyewe,”amesema Salum.
Amesema uchunguzi huo utafanywa na wataalamu wabobezi wa masuala ya miundombinu ya meli,mitambo na mifumo ya meli uundaji wake, jambo la faraja ni kwamba hakuna madhara kwa binadamu licha ya meli hiyo ya MV. Clarias kupinduka na kuzama.
Mkurugenzi huyo wa TASAC amesema juhudi za kuibua (kuitoa)majini meli hiyo ya MV.Clarias,zinaendelea kufanyika kwa kampuni ya Huduma za Meli (MSCL),ikishirikiana na kampuni za Songoro Marine na Mkombozi Transport, ikiibuliwa itapelekwa kwenye chelezo Mwanza Kusini kwa uchunguzi.
“Sababu za kiufundi meli kuzama,ni mashaka ya kufikirika,yawezekana ilikunywa maji (yaliiingia) ikiwa imetia nanga ikalalia upande mmoja,kwa nini iliingiza maji hicho ndicho tunachokitafuta,”amesema Salum.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa TASAC,watakachobaini katika uchunguzi huo wataishauri serikali hatua za kuchukua na taarifa itatolewa kupitia vyombo vya habari.
Naye Mkaguzi wa Meli TASAC ambaye ni Mtaalam wa Mitambo ya Meli, Mhandisi Samwel Chubwa,amedai kufahamu maji yaliingia melini kwa sasa ni vigumu, hivyo wapo hapa kubaini chanzo cha maji yaliingiaje melini.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Meli na Msanifu wa Vyombo vya Majini, Ally Hussein,amesema uundwaji wa meli hufanywa kulingana na michoro na hufuata matakwa ya sheria na kuzingatia usalama pia, muundo hutegemea meli itafanya kazi katika mazingira gani na majaribio hufanyika kuangalia usalama wa meli.
Meli ya MV.Clarias ilijengwa mwaka 1961 ,ina uwezo wa kubeba abiria 216 na tani kumi za mizigo, alfajiri ya kuamkia Mei 19, mwaka huu, majira ya saa 10 ilibainika kulalia upande mmoja ikiwa imetia nanga bandarini kabla ya kupinduka na kuzama majini.
Tukio hilo lilitokea ikiwa ni siku moja baada ya meli hiyo kurejea kutoka Kisiwa cha Gonziba,wilayani Muleba,Mkoa Kagera,ilishusha abiria na mizigo katika mwalo wa Kirumba, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na kuja kutia nanga Bandari ya Mwanza Kaskazini.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa TASAC, amesema wanajenga Kituo kikubwa cha Utafutaji na Uokozi katika eneo la Igombe mkoani Mwanza, kitakachokuwa na vifaa vya kisasa vya mawasiliano na uokoaji huku vingine vikitarajiwa kujengwa Geita na Kagera.
“Katika usimamizi wa vyombo vya majini tunaendelea kujiimarisha kiusalama kwa kudhibiti ujenzi wa vyombo na waendeshaji wake,kuboresha shughuli za ukoaji kwa kujenga kituo cha Uokozi na Utafutaji eneo la Igombe,” amesema.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania