November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtoto wa miaka mitatu adaiwa kuuwawa kwa kushambuliwa na fimbo na baba yake

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Alvin Fabian mtoto mwenye umri wa miaka 3, mkazi wa Kijiji cha Malya mkoani Mwanza amepoteza maisha baada ya kupigwa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi aitwaye Fabian Pauline(32) mkulima na mkazi wa kijiji cha Malya baada ya kumkuta mtoto huyo amejisaidia haja kubwa na kujipaka kinyesi.

Ambapo tukio la mauaji lilitokea Mei 09,2024 majira ya saa nne (10:00hrs) katika kijiji na Kata ya Malya, Tarafa ya Ibindo, Wilaya ya Kwimba mkoani hapa.

Akizungumzia tukio hilo,Mei 15, mwaka huu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP. Wilbroad Mutafungwa,ameeleza kuwa mwili wa Alvin Fabian umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi huku mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Huku tukio jingine la kikatili limetokea Mei 14,2024 majira ya saa 1 na dakika 43 usiku (19:43hrs) katika kijiji cha Kitumba Kata ya Kisesa, Tarafa ya Sanjo, Wilaya ya Magu mkoani hapa ambapo mtoto jinsia ya kike mwenye umri wa miaka 8, mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Kitumba na mkazi wa Kigungumule, alipigwa kwa ubapa wa panga, fimbo na mkanda wa suruali sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi aitwaye Ezron Macheya, miaka 47, Dereva na mkazi wa Kigungumule.

Hivyo kumsababishia maumivu makali sehemu za mapaja, mgongoni na mkono wa kulia kwa madai kuwa mtoto huyo amekuwa na tabia ya kuzurura mtaani usiku na kuchelewa kurudi nyumbani.

DCP.Mutafungwa ameeleza kuwa mtoto huyo, amepata michubuko sehemu mbalimbali za mwili wake na alipelekwa kituo cha afya Kisesa kwa ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri huku mtuhumiwa Ezron Macheya anaendelea kuhojiwa na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.

“Jeshi linatoa rai kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto wao pindi wanapo watuhumu kutenda makosa, badala yake watafute njia rafiki ya kuwaonya kuliko kutumia kipigo kwani madhara yake ni makubwa na ni kinyume cha sheria ya mtoto na sheria ya makosa ya jinai,”.

Sanjari na hayo DCP.Mutafungwa ameeleza kuwa katika tukio jingine lililotokea Mei 14,2024 majira ya 09:00hrs, katika mtaa wa Isenga “B”, Kata ya Kiseke, wilayani Ilemela, Amani Abeid Manyama (31), Mfanyabiashara na mkazi wa Tabata jijini Dar es salaam, alikutwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia waya wa kuanikia nguo kwenye mti wa Muembe nje kidogo ya nyumba ya babu yake aitwaye Berson Machumu Masuni,(67) alipokuwa akiishi.

Ameeleza kuwa inadaiwa kuwa Amani Abeid alikuwa anasumbuliwa na maradhi mbalimbali na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Mei 12,2024 ambapo Mei 13,2024 aliruhusiwa kutoka katika Hospitali hiyo baada ya kupata nafuu.

Ambapo ameeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni msongo wa mawazo uliotokana na kuugua kwa muda mrefu huku mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure kwa uchunguzi.

Hata hivyo jeshi hilo mkoani hapa linaendelea kutoa rai kwa wananchi kutafuta njia sahihi ya kutatua matatizo yanayowakabili kuliko kufanya maamuzi yasiyo na busara na kuzua taharuki kwa jamii.