December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

The Desk &Chair yamtua mama ndoo kichwani kwa milioni 20

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Magu

TAASISI ya The Desk & Chair Foundation,imekamilisha na kukabidhi mradi mkubwa wa kisima cha maji katika Kijiji cha Kitongosima wilayani Magu mkoani hapa ,utakaohudumia zaidi ya wananchi 2,000 wa kijiji hicho na wanafunzi 840 wa shule ya msingi Simakitongo.

Mradi huo umegharimu kiasi cha milioni 20,utawanufaisha watumishi na watoto 75 wenye changamoto ya mgongo wazi na vichwa vikubwa wanaolelewa katika Kituo cha Nyumba ya Matumaini cha Child Help Tanzania ikiwemo mifugo ya ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Akikabidhi mradi huo wa kisima cha maji Mei 12,2024 Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation,Dkt.Alhaji Sibtain Meghjee,amesema kisima hicho kitaondoa adha ya muda mrefu ya kusaka maji waliyokuwa wakiipata wananchi wa Kijiji cha Kitongosima na mifugo yao.

“Mradi una uwezo wa kuzalisha lita 10,000 za maji na mfumo wa mtandao wa maji tunaokabidhi ni pamoja na mitambo ya Solar (umemejua),manteki mawili ya maji,nguzo mbili za matenki na sehemu ya kunyweshea mifugo,”amesema.

Dkt.Alhaji Meghjee amesema mradi huo umeonesha ufanisi mkubwa kwa wananchi kipekee pia walifikiria mifugo yao na hivyo wameijengea sehemu safi ya kunywa maji kwa mwaka mzima na kuwataka wananchi hao kutunza miundomboni hiyo iwahudumie kwa muda mrefu.

Amewashukuru wafadhili wa mradi huo wa maji,serikali,uongozi wa kijiji na wananchi kwa ushirikiano uliowezesha kuukamilika kwa ubora kulingana na thamani ya fedha iliyotumika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya akinamama wa Kitongosima,Nyangeta Magoti na Scolastica Magubu,wamesema mradi uko vizuri sasa wameondokana na adha ya kuzunguka usiku na mchana kutafuta huduma ya maji.

“Eneo hili lilikuwa na shida kubwa ya maji na wananchi waliteseka kusaka huduma hii wakiamka usiku,njiani walikutana na wanyama hasa fisi lakini The Desk & Chair Foundation,kuwekeza fedha zao kutekeleza mradi huu mkubwa,wamewatua akina mama ndoo kichwani,”amesema Nyangeta.

Scolastica amesema walikuwa wakitoka saa 9 usiku kutafuta maji na kurudi asubuhi saa 4,walitumia muda mwingi kupata huduma ya maji hali iliyosababisha migogoro na kuhatarisha ndoa zao, hivyo mradi huo utaimarisha familia kwani wamefikishiwa huduma karibu na watapata fursa ya kufanya shughuli za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.


“Mradi huu wa maji ni mkombozi mkubwa kwetu wananchi hasa kina mama,tulikuwa tukitembea zaidi ya kilometa tano kutafuta maji,wakati mwingine tulitoka usiku na kurudi asubuhi,jambo hilo lilihatarisha ndoa zetu na hata maisha,”amesema.

Kwa upande wake mwanafunzi wa Shule ya Msingi Simakitongo,Rosemary Avit,amesema ukosefu wa maji shuleni uliwakwamisha baadhi yao kuhudhuria masomo wakipeana zamu ya kuteka maji,tatizo lililowarudisha nyuma kielimu.

Amesema shule hiyo haikuwa na huduma ya majisafi na salama licha ya serikali kuboresha miundombinu ya elimu kwa kuleta vitabu,madawati na kupanda miti ya matunda na vivuli kutunza mazingira,wanashukuru kupata maji ya bomba,changamoto iliyobaki ni uhaba wa vyumba 10 vya madarasa,nyumba nne za walimu,vyoo matundu 14 na madawati 200.

Mtendaji wa Kijiji cha Kitongosima,Majige Masalamali ameishukuru The Desk & Chair Foundation na wadau wa maendeleo kuunga mkono dhamira ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.

Sheikh wa Bilal Muslim Kanda ya Ziwa,Sheikh Hashim Ramadhan amewashukuru wafadhili wa mradi huo akisema wameingiza furaha kwa jamii kwa zawadi ya maji pia, Mtume Muhammad S.A.W na Mwenyezi Mungu.