November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni ujenzi wa maabara masomo ya sayansi yashika kasi Musoma Vijijini

Fresha Kinasa, Timesmajira Online, Musoma

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara Prof. Sospeter Muhongo ameanzisha kampeni ya ujenzi wa maabara tatu (3) za masomo ya Sayansi kwa kila sekondari ilipo jimboni humo zikiwemo za binafsi.

Maabara zinazojengwa ni za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia lengo ni kuhakikisha taifa linaendelea kuwaandaa wasomi watakao endelea kuleta mageuzi chanya katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini.

Hayo yamesemwa kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo Mei 10, 2024 ambayo imeeleza kuwa wachangiaji wa ujenzi wa maabara hizo ni serikali, mfuko wa Jimbo, Mbunge, Wanavijiji na Viongozi wao wakiwemo Madiwani.

Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, hadi leo hii lina jumla ya Sekondari 28 Kati ya hizo, 26 ni za serikali na 2 ni za binafsi huku sekondari mpya kumi zikijengwa jimboni humo.

Mafanikio ya kampeni hiyo yametajwa kuwa ni pamoja na Sekondari zenye maabara tatu za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia ni saba (7) ambazo ni Bugwema, Bwai, Ekwabi (Wanyere), Ifulifu, Kiriba, Mugango na Nyakatende.

Pia, Sekondari zenye maabara mbili (2) na zinakamilisha maabara ya tatu ni tano (5) ambazo ni Bulinga, Etaro, Makojo, Rusoli na Suguti.

Huku sekondari kumi na sita (16) zilizosalia zina maabara moja (1) hadi mbili (2) na zinaendelea na ujenzi wa maabara zilizokosekana.

“Zipo Sekondari tatu (3) ambazo hazina maabara hata moja, nazo hizi zimeanza ujenzi wa maabara tatu,wazaliwa wa Musoma Vijijini na wadau wengine wa maendeleo tanaomba kuchangia ujenzi huo,”.

Nao Wananchi jimboni humo, wamesema kukamilika kwa maabara tatu za masomo ya Sayansi kwa kila sekondari jimboni humo kutaongeza chachu kwa wanafunzi kupenda masomo hayo na kuyasoma kwa ufanisi.

Huku wakisema yanamchango mkubwa katika kuleta mageuzi chanya ya maendeleo ya sekta mbalimbali katika Taifa.